advanced Search
KAGUA
5612
Tarehe ya kuingizwa: 2019/01/24
Summary Maswali
kwa mtazamo wa Qur-ani, ni amali gani zinazoweza kuharibu na kubatilisha amali njema zenye kuthaminiwa?
SWALI
kwa mtazamo wa Qur-ani, ni amali gani zinazoweza kuharibu na kubatilisha amali njema zenye kuthaminika?
MUKHTASARI WA JAWABU
Ndani ya Qur-ani na Riwaya mbali mbali, kuna mafunzo mbali mbali yenye kuwafahamisha waja masharti ya mwanzo yanayosababisha  kukubaliwa amali zao, na masharti msingi yaliyotajwa katika mafunzo hayo ni kumuamini Mola, kujiepusha na shirki pamoja kuto ritadi, na bila ya kuwepo misingi hiyo Mola hatozikubali aina zozote zile za amali njema zitakazotendwa na waja wake. Ama kuhusiana na zile amali zenye kubatilisha amli njema za waja, ni kama vile kuacha sala, kusimbulia na kumletea mja bughudha baada ya kumtendea mema, pamoja na kuto ridhika na hali au matokeo ya misiba na mitihani ya Mola n.k.
  Nasi katika makala hii tunakusudia kuyafafanua mambo haya vya kutosha kabisa katika jawabu kamili zitakazofuatia baadae, kinachotaka kuzingatiwa hapa ni kwamba: kuna fungamano la moja kwa moja baina ya kudumu kwa imani na kuto haribika kwa amali njema, kwani mdhamini pekee wa kuyadhamini matendo mema na kuyahifadhi matendo hayo yasiharibike, ni kule mja kubaki na kusimama kidete katika imani yake.
JAWABU KWA UFAFANUZI
Qur-ani na Riwaya mbali mbali zilipokuwa zikizungumzia yale madhambi yanayo sababisha kuharibika kwa matendo mema, imetumia ibara ya (kuporomoka kwa matendo mema) ikimaanisha kuharibika na kubatilika kwa amali njema, ibara ambayo ni yenye kutokana na neno (حبط) lenye maana ya kuporomoka. Kwa hiyo kabla ya sisi kuanza kulijibu swali lililo ulizwa na muulizaji wetu, kwanza kabisa inatubidi tulifafanue neno hili, kisha kuainisha aina za matendo yenye kubeba maana kamili ya makusudio yaliyokusudiwa na Qur-ani pamoja na Riwaya katika kulitumia neno hilo, na paada ya kufanya hivyo, hapo tena tataelekea katika kubainisha umuhimu wa kuyahifadhi matendo mema.
 
Maana ya neno (حبط):
Neno (حبط) lina maana ya kubatilika kwa matendo, na neno hili linapotumika ndani ya Qur-ani pamoja na Riwaya mbali mbali huwa linamaanisha kufutika au kufutwa kwa ujira au thawabu ambazo zilikuwa zikimsubiri mtendaji wa amali hizo.[1] Pia neno (حبط) lina maana ya kufisidika kwa amali na kupoteza thamani yake.[2]
Kuna matendo maalumu yaliyotajwa ndani ya maandiko ya Qur-ani pamoja na Riwaya, ambayo huwa ni sababu ya kubatilika kwa matendo mema, yaani matendo hayo hubatilisha ule ujira wa matendo mema aliyoyatenda mja katika zama fulani. Na fuatao hapa  ni utafiti juu ya matendo hayo:
NENO (حبط) NDANI YA QUR-ANI
Neno hili limekuja mara kumi na sita ndani ya Qur-ani huku likiwa katika hali ya minyambuko mbali mbali yenye kumaanisha uharibikaji na kufusidika kwa amali njema, nasi hapa tutaashiria baadhi ya matendo yenye kubatilisha amali njema na namna ya neno hili lilivyotumika ndani ya ibara zenye kuashiria matnedo hayo:
1- Kumkufuru Mungu na kumshirikisha:
  • [3] "مَنْ يَكْفُرْ بِالْإيمانِ فَقَدْ حَبِطَ عَمَلُهُ وَ هُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخاسِرينَ"
Maana yake ni kwamba: (Na yeyote yule atakayeikufuru imani ya dini ya Kiislamu, amali zake zitaharibika na kubatilika, na siku ya Kiama yeye atakuwa ni miongoni mwa waliokula hasara.)
  • [4] "ما كانَ لِلْمُشْرِكينَ أَنْ يَعْمُرُوا مَساجِدَ اللَّهِ شاهِدينَ عَلى‏  أَنْفُسِهِمْ بِالْكُفْرِ أُولئِكَ حَبِطَتْ أَعْمالُهُمْ وَ فِي النَّارِ هُمْ خالِدُون‏".
Maana yake ni kwamba: (Washirikina hawastahili kuimarisha misikiti ya Mwenye Ezi Mungu hali ya kuwa wao ni wenye kuushuhudia ukafiri wao, hao tayari amali zao zimesha haribika na kubatilika nao watadumu ndani ya moto wa Jahannam).
Aya mbili hizi tulizozitaja hapa, zimebainisha wazi wazi ya kuwa: kumkufuru Mungu na kumshirikisha, ni miongoni mwa matendo yenye kusababisha kubatilika na kuharibika kwa amali njema, na amali za makafiri na washirikina haziwezi kudumu na kuthibiti kama Aya hizi zilivyo tubainishia.
2- Unafuki:
"وَ يَقُولُ الَّذينَ آمَنُوا أَ هؤُلاءِ الَّذينَ أَقْسَمُوا بِاللَّهِ جَهْدَ أَيْمانِهِمْ إِنَّهُمْ لَمَعَكُمْ حَبِطَتْ أَعْمالُهُمْ فَأَصْبَحُوا خاسِرين‏" [5]
Maana yake ni kwamba: (Wale walio amini wanasema: je hawa (wanafiki) ndiwo wale waliokula kiapo kwa ajili ya kutilia mkazo kuwa wao wapo pamoja na nyinyi?! Sasa amali zao zimesha batilika na kuharibika na tayari wao wameshakula hasara).
3- Kuzikanusha Aya na dalili za Mwenye Ezi Mungu na kuikanusha siku ya malipo:
"وَ الَّذينَ كَذَّبُوا بِآياتِنا وَ لِقاءِ الْآخِرَةِ حَبِطَتْ أَعْمالُهُمْ هَلْ يُجْزَوْنَ إِلاَّ ما كانُوا يَعْمَلُون‏" [6]
Maana ya Ayah hii ni kwamba: (Na wale waliziokanusha Aya zetu na wakakanusha kuwa wao watakabiliana na siku ya malipo, hao amali zao zimebatilika, jee hivi kuna malipo mengine watakayolipwa zaidi ya yale yaendayo sawa na matendo yao waliyoyatenda?!).
NENO (حبط) NDANI YA RIWAYA
  1. Kuacha sala bila ya maradhi wala dharura inayokubalika
Ubeid bin Zurara kuhusiana na hilo anasema: mimi nilimuuliza Imamu Saadiq (a.s) maana na tafsiri ya Aya isemayo kuwa: (Na yeyote yule atakayeikufuru imani ya dini ya Kiislamu, huyo amali zake zitakuwa ni zenye kubatilika.)[7] Yeye (a.s) alinijibu kwa kusema: mkusudiwa katika Aya hii ni yule aliyeikubali haki na kuyakubali matendo yanayoshikamana na haki hiyo, kisha matendo yake yakawa ni kinyume na imani yake ilivyo, au akawacha kuyatenda yale matendo yaendayo sawa na imani hiyo. Hapo mimi niliuliza: ni kiwango gani cha kuacha matendo kinasababisha mtu kuingia katika kundi hilo? Hivi amali za mtu zitabatilika iwapo yeye atawachana na amali zote? Yeye (a.s) akajibu: miongoni mwa yale yenye kubatilisha amali njema, ni kule mtu kuacha sala bila ya dharura yenye kukubalika kisheria.[8]
  1. Kutokuwa na uhakika juu ya misingi mikuu ya dini
Mmoja kati ya wafuasi wa Imamu Saadiq (a.s) ajulikanaye kwa jina la Mufadhal amesema kuwa: yeye amemsikia Imamu Saadiq (a.s) akisema kwamba: mtu yeyote yule atakayeyasimamisha matendo yake juu ya msingi au misingi ya dini asiyo na uhakika nayo, Mola atazibatilisha amali zake, kwani hoja za Mwenye Ezi Mungu ziko wazi kabisa.[9]
Allaama Majlisiy (r.a) ameifafanua Riwaya hii kwa kusema: haimjuzii yule mwenye uwezo kuufikia uhakika na yakini juu ya misingi ya dini, kutenda amali zake pasi na kuifikia yakini hiyo, na maana ya ile ibara iliyosema kuwa (hoja za Mwenye Ezi Mungu ziko wazi), ni kwamba: yeyote yule atakaye utafuta ukweli na uhakika wa misingi ya dini, bila shaka atalifikia lengo hilo, naye hatobaki katika shaka juu ya hilo.[10]
  1. Kauli ya mwanamke atakapomwambia mumewe kuwa yeye hakupata kheri yoyote ile kutoka kwa mume huyo
Ingawaje mwanamke huwa hawajibikiwi na kazi za ndani ya nyumba kama vile kupika, kufua, kusafisha nyumba na mengineyo, lakini mara nyingi wanawake huonekana kufanya kazi hizo kwa nia safi kwa ajili ya kulikuza na kuliboresha fungamano lilipo baina ya mume na mke, na Mola Mtukufu huwaandalia malipo makubwa wanawake wenye kuwasaidia waume zao, lakini ni vizuri wanawake kufahamu kuwa: iwapo matendo yao hayo ya kuwasaidia waume zao yatafuatiliwa na maudhi au masimbulizi, hapo Mola wao atazibatilisha amali hizo njema ambazo wao walizitenda kisha wakawa wanawasumbua na kuwasimbulia waume zao kwa kutokana na msaada wao wa kuwasaidia waume zao. Kuhusiana na hilo, Imamu Saadiq anasema: mke yeyote yule atakayemwambia mumewe: (mimi sijaona kheri yoyote ile kutoka kwako), amali za mwanamke huyo zitabatilika na kufisidika ujira wake.[11]
  1. Kuukana uimamu wa Ali (a.s)
Ibnu Hamza amesema kuwa: mimi nilimuuliza Imamu Baaqir (a.s) kuhusu tafsiri na maana ya ile Aya isemayo:
 "وَ مَنْ يَكْفُرْ بِالْإِيمانِ فَقَدْ حَبِطَ عَمَلُهُ وَ هُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخاسِرِين"
Akanijibu kwa kusema: maana ya ndani ya Aya hii ni kwamba: yule atakayeukanusha uimamu wa Ali (a.s), amali zake zitabatilika naye atakuwa miongoni mwa wenye kukhasirika, kwani dhihiriko na picha kamili ya imani inapatikana kwa Ali (a.s), naye ndiye mwenye picha kamili ya imani.[12]
Kutokana na utafiti huu, inaonekana kwamba: suala la kubatilika kwa matendo, huwa si jambo lenye kulenga baadhi ya matendo yenye kuhusiana na mrengo maalumu bila ya kuihusisha mirengo mengine, bali suala hili huwa linaingiza ndani yake aina zote zile za matendo mema yalioko katika nyanja na mirengo mbali mbali ya kijamii, kibinafsi, kiimani pamoja na matendo mengine yanayo husiana na tabia njema.
Tukizingatia kuwa suala la kubomoka na kufutika kwa matendo ya mwanaadamu, si suala tu lenye kuhusiana na matendo mema, bali vile vile kuna amali maalumu zinazoweza kufuta athari za matendo maovu, hivyo basi inatubidi pia sisi tutoe ufafanuzi kwa kiasi fulani kuhusiana na suala hili.
  Linalotakiwa kuzingatiwa na kueleweka vizuri na kila mmoja wetu, ni kuwa: kuna amali maalumu zinazosababisha kufutika kwa athari za matendo maovu, na pia si tu uwezekano wa kufutika kwa athari au matendo maovu ni jambo linalowezekana, bali pia kuna uwezekano wa amali fulani kuja kuufuta ujira wa amali mbaya na badala yake mtendaji wa amali hizo akalipwa malipo mema, na amali zake kugeuzwa kuwa ni miongoni mwa mambo mema, na ifuatayo hapa ni mifano ya amali na matendo yawezayo kufanya kazi hiyo:
  1. Kusali sala za wajibu (za faradhi)
"وَ أَقِمِ الصَّلاةَ طَرَفَيِ النَّهارِ، وَ زُلَفاً مِنَ اللَّيْلِ، إِنَّ الْحَسَناتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئات‏"
Maana ya Aya hii ni kwamba: (Na simamisha sala ndani pande (ncha) mbili za mchana na ndani ya baadhi ya masaa ya usiku, kwa hakika amali njema ni zenye kufuta amali mbovu).[13]
  1. Kujiepusha na madhambi makuu
  1. "إِنْ تَجْتَنِبُوا كَبائِرَ ما تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنْكُمْ سَيِّئاتِكُمْ"
Maana yake ni kwamba: (Iwapo mtajiepusha na madhambi makuu mnayokatazwa nayo, basi tutakusameheni madhambi yenu).[14]
  1. "الَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبائِرَ الْإِثْمِ وَ الْفَواحِشَ إِلَّا اللَّمَمَ، إِنَّ رَبَّكَ واسِعُ الْمَغْفِرَةِ"
Maana yake ni kwamba: (Wale wenye kujiepusha na madhambi makuu pamoja na mambo machafu, ila tu wakawa wameteleza katika baadhi ya makosa madogo madogo, kwa hakika Mola wako ni Mukuu wa kusamehe).[15]
Kwa kutokana na umuhimu wa mtu kudumu katika imani pamoja na kuihifadhi imani aliyokuwa nayo, ni muhimu basi sisi tutoe baadhi ya maelezo na ufafanuzi kuhusiana na jambo hili:
 
 Moja kati ya masuala muhimu yaliyotiliwa mkazo ndani ya Qur-ani na Riwaya mbali mbali kuhusiana na amali za mwanaadamu, ni kule mtu kuchukua juhudi za hali ya juu katika kutenda mema na kuyalinda matendo yake baada ya kuyatenda, kwani bila ya kufanyika kwa juhudi kuhusiana na hilo, yawezekana sisi tukakabiliwa na natija isiyo ridhisha huku sisi tukiwa katika subira ya kusubiri ujira wa matendo yetu mema.
 Ndani ya Hadithi za Mtume (s.a.w.w) kumetajawa fadhila nyingi kuhusiana na zile dhikri nne maarufu zinazotajwa baada ya kila sala ya faradhi, Naye (s.a.w.w) kuhusiana umuhimu wa dhikri, amesema kuwa: kila dhikri moja itakayotajwa na mja, husababisha Mola kumlipa mja huyo kwa kumuoteshea yeye mti mmoja ndani ya Pepo yake, baada ya Yeye (s.a.w.w) kutoa taarifa hii, akatokea mtu mmoja aliyesema: basi sisi tuna idadi iliyoje ya miti huko Peponi! Hapo Mtume (s.a.w.w) akasema: ndiyo, lakini tahadharini msije kupeleka moto utakao iunguza miti hiyo, kisha Yeye (s.a.w.w) akaisoma Aya ifuatayo: (يـا ايها الذين امنوا اطيعوا اللّه و اطيعوا الرسول و لا تبطلوا اعمالكم)
Maana yake ni kwamba: (Enyi mlioamini mtiini Mola wenu na mtiini mjumbe wake na wala msizibatilishe amali zenu) .[16]
Mwisho wa ufafanuzi.
Twataraji maelezo yetu yatawanufaisha wasomaji wa makala hii.
 
 

[1] Al-Sihaahu cha Ismail bin Hammaad Al-Jawahiriy, juz/3, uk/1118, chapa ya Darul-Ilmi, Beirut, mwaka 1990 Miladia.
[2] Al-Misbahul-Muniir cha Ahmad bin Muhammad Al-Fayyumiy, uk/118.
[3] Aya ya tano ya Suratul-Maaida.
[4] Aya ya 17 ya Suratut-Tawba.
[5] Suratul-Maaida, Aya ya 53.
[6] Suratul-Aa’raaf, Aya ya 147.
[7] Suratul-Maaida, Aya ya 5.
[9] Rejea rejeo lililopita, juz/2, uk/400.
[10] Mir-aatul-Uquul cha Muhammad bin Baqir Majlisiy, juz/11, uk/186, chapa ya Darul-Kutubil-Islamiyya, Tehran, mwaka 1404 Hijiria.
[11] Wasaailush-Shia, cha Muhammad bin Hasan Al-Majlisiy, juz/20. uk/162, chapa ya taasisi ya Aalul-Bait, Qum, mwaka 1404 Hijiria.
[12] Biharul-Anwaar, cha Muhammad bin Baaqir Al-Majlisiy, juz/35, uk369, chapa ya Intishaaraat-Kitaabkhaaneye-Islaamiyye, Tehran, mwaka 1362 Shamsia.
[13] Suratu Huud, Aya ya 114.
[14] Suratun-Nisaa, Aya ya 31.
[15] Suratun-Najmi, Aya ya 32.
[16] Suratu Muhammad, Aya ya 33, Al-Aamaali, cha Muhammad bin Ali Aaduuq, juz/1, uk/607, chapa ya Intishaaraat-Kitaabkhaaneye-Islaamiyye, Tehran, mwaka 1362 Shamsia.
 
TARJAMA YA JAWABU KATIKA LUGHA NYENGINE
MAONI
Idadi ya maoni 0
Tafadhali ingiza thamani
mfano : Yourname@YourDomane.ext
Tafadhali ingiza thamani
<< Niburute.
Tafadhali ingiza kiasi sahihi ya usalama Kanuni

MPANGILIO WA KIMAUDHUI

MASWALI KIHOLELA

YALIYOSOMWA ZAIDI