Please Wait
14763
- Shiriki
Masiku yasiyofaa kufunga saumu mbele ya imam Abu Hanifa ni: siku ya idi ndogo na idi kubwa, pia kufunga siku ya mwezi 11, 12 na 13 ya mwezi wa Dhil-hijja, pia kufunga ndani ya idi pili hadi nne za idi ya mfunguo tatu.
Funga zisizofaa kwa mtazamo wa imam Shafi ni: kufunga siku ijulikanayo kwa jina la yaumu shaka, kufunga siku ya idi ndogo na kubwa, vile vile kufunga ndani ya idi pili hadi nne za idi ya mfunguo tatu, iwe mtu yupo kwenye ibada ya hija au nyumbani, kufunga kabla ya kuingia mwezi wa Ramadhani kwa siku moja au mbili pia ni haramu, kufunga kwa kuanzia nusu ya pili ya Shaabani iwapo utakuwa hukuanza kufunga tanga mwanzo wa mwezi huo, ila tu unaruhusiwa kufunga ndani ya masiku hayo pale utapokuwa umeweka nadhiri ya funga au kwa mwanamke ambaye ana dharura ya kuzilipa funga zake zilizompita kwa kutokana na dharura za uke (hedhi).
A - funga zisizofaa mbele ya imam Abu Hanifa ni kama ifuatavyo:
1- haifai kufunga katika siku ya kuchinja katika ibada ya hija: na iwapo mtu ataweka nadhiri ya kufunga katika siku hiyo, nadhiri yake haitohesabiwa kuwa ni nadhiri inayokubalika, kwa kule kuharamika kwa saumu ndani ya siku kama hiyo, na ni maasi kufunga ndani ya siku hiyo.[1]
2- kufunga siku ya idi ndogo na idi kubwa pamoja na siku tatu baada ya Idul-adh-haa ambayo ni idi inayofanyika baada ya ibada ya hija haifai kufunga ndani yake, na kufunga ndani ya siku tatu hizo ni Makruhu iliyo kubwa kabisa (مکروه تحریمی) isipokuwa kwa yule atakayekuwepo ndani ya ibada ya hija.[2]
3- ni Makruhu kufunga ndani ya masiku ya Ayyaami tashriiq, nayo ni mwezi 11,12 na 13 ya Dhil-hijja.[3]
Mahanafi (watu wa madhehebu ya Hanafiy), hulitumia neno (مکروه تحریمی), wakimaanisha tendo lililo karibu na uharamu.[4]
B- funga zisizofaa mbele ya imam Shafi ni:
1- kufunga ndani ya siku ya Yaumu shaka ni Haramu hadi mwezi uonekanae.[5]
2- ni Haramu kufunga siku ya Idul-Fitr na Idul-Adh-haa, ambazo ni zenye kujulikana kwa jina la siku kuu ndogo na siku kuu kubwa, pia ni Haramu kufunga siku tatu baada ya Idul-Adh-haa, wala hakuna tofauti baina ya yule aliyekuwemo ndani ya ibada ya hija au yule asiye kuwepo kwenye ibada hiyo.[6]
3- ni Haramu kufunga siku moja au mbili kabla ya kuingia mwezi wa Ramadhan.[7]
4- ni haramu kufunga kwa kuazia nusu ya pili ya Shaabani iwapo mtu atakuwa hakuanza kufunga tokea mwanzoni mwa Shaabani, kwa hiyo hakutokuwa na tatizo kwa yule aliye anza kuufunga mwezi huo tokea mwanzoni mwake na kuuendeleza hadi uwezo wake utavyomruhusu.[8]
5- ni haramu kufunga saumu kwa mtu ambaye saumu kwake ni yenye kumletea madhara, kiasi ya kwaba iwapo atafunga basi aweza kupoteza kimoja kati ya viungo vya mwili wake, au itakapo khofiwa kuhiliki mtu huyo kwa kutokana na kufunga.[9]
6- ni haramu mke kufunga saumu ya Sunna bila ya idhini ya mumewe, iwapo funga hiyo itasababisha kupotea kwa haki za mume huyo, hiyo ni kwa sababu mke anatakiwa kufuata amri za mumewe.[10]
C- funga zisizofaa kwa mujibu wa mtazamo wa imam Maalik:
1- ni haramu kufunga kabla ya kuonekana kwa mwezi wa Ramadhani hadi mwezi uandame, hata kama mwezi wa Shaabani utakuwa umeshazidi zaida ya siku thalathini.[11]
2- ni Haramu kwa mwanamke kufunga funga ya Sunna bila ya idhini ya mumewe, iwapo funga hiyo itasababisha kupotea kwa haki za mume huyo, hiyo ni kwa sababu mke anatakiwa kufuata amri za mumewe.[12]
3- ni Haramu kufunga ndani ya siku ya idi ya baada ya Ramadhani na idi ya Mfunguo tatu.[13]
4- ni Haramu kufunga mwezi11, 12 na 13 za mwezi wa Dhul-Hijja, ambazo ni baada ya idi tu.[14]
5- ni Haramu kufunga siku ya shaka (yaumu shaka), yaani siku ambayo inatiliwa shaka na haieleweki kuwa ni ya mwezi wa Shaabani au Ramadhani.[15]
[1] Kitabu Tabyinul-Haqaaiq wa haashiatu Al-Shabliy, mlango wa funga, kipengele kisemacho (فَصْلٌ نَذَرَ صَوْمَ يَوْمِ النَّحْرِ) cha Fakhrudi-diin Al-Zai-iliy Al-Hanafiy, Uthman bin Ali bin Muhjin Al-Baari-iy.
[2] Alfiqhu alaa madhaahibil-arba-a wa madhabu Ahli-bait, juz/1 uk/720, chapa ya kwanza ya Daruth- thaqalain ya mwaka 1419 Hijiria, pia Al-fiqhu alaa madhaahibul- khamsa cha Muhammad Jawad Al-Mughniya, juz/1 uk/160, chapa ya kwanza ya Daru tayyaril-jadiid-Darul- Jawad Beirut, mwaka 1421 Hijiria.
[3] Alfiqhu alaa madhaahibil-khamsa, juz/1, uk/161.
[4] Rejea kitabu kilichopita, uk/160.
[5] Majmu-u fatawa wa rasaail fadhilatu sheikh Muhammad bin Saleh Al-Uthaimin, cha Muhamma bin Saleh bin Muhammad Al-Utahaimin, mlango wa funga, kipengele cha, funga ya kujikaribisha kwa Mola, ambacho ni kitabu kilichoandikwa kwa Kiarabu, na muongozo wake wa rejeo hii kwa Kiarabu ni kama ifuatavyo:
. کتاب الصیام، « صیام التطوع »، مسائل من کتاب الفروع، المسألة الاولی، القول الخامس.
[6] Fiqhi alaa mdahahibil-arba-a wa madhabi Ahlul-Bait, juz/1, uk/720, pia Fiqhu alaa mdahahibil-khamsa, juz/1, uk/160.
[7] Fiqhu alaa mdahahibil-arba-a wa madhabi Ahlul-Bait, juz/1, uk/726.
[8] Rejea ki kitabu kilichopita.
[9] Rejea kitabu hicho hicho, uk/727.
[10] Kitabu kilichopita, uk/720 hadi 721, pia uk/727. Pia kitabu Fiqhu alaa mdahahibil-khamsa, juz/1, uk/161.
[11] Majmu-u fatawa wa rasaail Fadhilatu sheikh Muhammad bin Saleh Al- Uthaimin, na bayana yake kwa kiarabu ni kama ifuatavyo:
مجموع فتاوى ورسائل فضيلة الشيخ محمد بن صالح العثيمين، کتاب الصیام، « صیام التطوع »، مسائل من کتاب الفروع، المسألة الاولی، القول الخامس.
[12] Alfiqhu alaa mdahahibil-arba-a wa madhabi Ahlul-Bait, juz/1, uk/720 hadi 721, pia uk/727, pia rejea kitabu Alfiqhu alaa madhahibil-khamsa, juz/1, uk/161.
[13] Kitabu kilichopita, uk/720, pia kutabu kilichopita, uk/160.
[14] Kitabu kilichopita, uk/160 hadi 161.
[15] Alfiqhu alaa mdahahibil-arba-a wa madhabi Ahlul-Bait, juz/1, uk/720.