advanced Search
KAGUA
23991
Tarehe ya kuingizwa: 2012/05/05
Summary Maswali
vipi madhehebu manne ya Ahlu-Sunna yalipatikana, na ilikuwaje mlango wa ijitihadi wa madhehebu hayo ukafungwa?
SWALI
ni vipi madhehebu manne ya Ahlu-Sunna yalipatikana, na kwa nini mlango wa ijitihadi ndani ya madhehebu hayo ukafungwa? Na ni nani kwa mara ya kwanza kabisa aliye ufungua mlango wa ijitihadi, kwa upande wa Ahlu-Sunna?
MUKHTASARI WA JAWABU

Mafunzo na fiqhi ya Kiislamu yaligawika sehemu mbili tokea ndani ya kipindi cha mwanzo cha tarehe ya Kiislamu baada tu ya kufariki Mtume (s.a.w.w), kipindi ambacho kilikuwa ni kipindi cha mzozo katika suala la nani ashike ukhalifa baada ya Mtume (s.a.w.w), hapo kukazaliwa aina mbili za fiqhi: ya kwanza ni ile fiqhi iliyotegemea elimu ya watu wa kizazi cha Mtume (s.a.w.w), waliojulikana kwa jina la Ahlul-Bait (a.s), na ya  pili ni ile fiqhi iliyoegemea kwenye mgongo wa masahaba mbali mbali pamoja na waliokuja baada yao, ambao ni miongoni mwa wafuasi wao, na gurupu hili lililozaa aina hii ya pili ya kifiqhi, lilijulikana kwa jina la Ahlu-Sunna.

Kuzaliwa kwa aina mbali mbali za maswali ya kisheria, kulisonga mbele siku baada ya siku, na jambo lililokoza zaidi rangi yake baada ya watu kutoka nchi mbali mbali kusilimu, tokeo ambalo lilionekana kuwa ni lenye mawimbi makali mno ndani ya zama za ufunguzi wa nchi mbali mbali uliofanywa na Waislamu kwa nia ya kuusambaza utamaduni wa Kiislamu, hivyo basi mawimbi hayo ya usambazaji wa dini na utamaduni wa Kiislamu, yalizaa aina mpya za maswali mengi yenye mfumo mpya kwenye nyanja za kisheria na kitamaduni. Yaani ninachotaka kukisema hapa ni kwamba: kuanzia mwanzoni mwa karne ya pili Hijiria hadi kufikia mwanzoni mwa karne ya nne Hijiria, ndicho kipindi ambacho ndani yake fiqhi ya Ahlu-Sunna ilichipuka vyema na kupea ndani yake. Kipindi hicho ndicho kilicho zaa madhehebu manne ya Ahlu-Sunna. Ijitihadi ndani ya nyanja zote za kifiqhi, iliendelea ndani ya madhehebu yote ya Kisunni. Na suala hili liliendelea ndani ya madhehebu ya Ahlu-Sunna hadi kufikia mwaka 665 Hijiria, lakini kwa kutokana na sababu maalumu, madhehebu mengine ya Kisunni yakawa ni yenye kupuuzwa na kutopewa thamani, na nyadhifa zote zenye kuhusiana na mambo ya kifiqhi ndani ya jamii, kama vile uimamu wa misikiti, ukadhi na mengineyo, zikawa zimetawaliwa na watu wenye kufungamana na moja kati ya madhehebu manne tu ya Kisunni. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumeanza kusikika minong’ono juu ya kufunguliwa mlango wa ijitihadi kwa mara nyengine tena. Hivi sasa kumekuwepo gurudumu maalumu lililoanza kutaka kufanya ijtihadi ndani ya moja kati ya madhehebu ya Kisunni, na hatimae kuupanua zaidi mlango huo wa ijitihadi, hadi kuyaingia madhehebu yote ya Kisunni ndani ya kazi yao hiyo ya ijitihadi. Mabadiliko ya haraka na ya kila dakika ndani ya maisha ya mwanaadamu anayeishi ndani ya karne ya leo, ndiyo yaliyowalazimisha wafuasi na wanazuoni wa madhehebu ya Kisunni kuufungua tena mlango wa ijitihadi kwa mara nyengine tena baada ya mlango huo kufungwa kwa muda wa miaka mingi iliyopita.

JAWABU KWA UFAFANUZI

Usajili wa hukumu za kisheria ulianza tangu zama za Mtume (s.a.w.w), na kuendelea ndani ya kipindi chote cha maisha yake. Kwa mtazamo wa madhehebu ya Kishia ni kwamba: majukumu yote yale ya kuzibainisha hukumu za kisheria za kibinafsi na za kijamii, pamoja na kutoa picha nzima ya maisha na nyenendo za Mtume (s.a.w.w), yako kwenye mkono wa Ahlul-bait (a.s), kwa hiyo wao ndiwo wenye mamlaka ya kuzifafanua sheria pamoja na nyenendo za Mtume (s.a.w.w) kwa ajili ya kuwaongoza watu wengine.

Ama kwa mtazamo wa wafuasi wa madhehebu ya Kisunni ni kwamba: mamlaka hayo ni milki ya masahaba, nao ndiwo wenye jukumu la kuwaongoza watu katika misingi ya kidini na kisheria.  Ubainishaji wa hukumu za kisheria pamoja kuutafakari mfumo mzima wa fiqhi, Sunna za Mtume, pamoja maisha yake (s.a.w.w) kwa ujumla, lilikuwa ni suala lililoshikwa na masahaba hadi kufikia karibu ya mwaka wa 40 Hijiria.[1] Na baada ya kipindi hicho ambapo bado baadhi ya masahaba walikuwa wako hai, lakini aghalabu ya wanazuoni wa fani fiqhi (mafaqihi), walikuwa si miongoni mwa masahaba, wadhifa wa kuitangaza na kuichambua dini na sheria zake, ukawa katika mikono ya taabiina (wafuasi wa masahaba), jambo hilo lilianza katika zama za mwishoni mwa karne ya mwanzo Hijiria hadi mwanzoni mwa karne ya pili Hijiria.[2]

Zama za kudhihiri na kuchomoza kwa madhehebu ya kifiqhi ya Kisunni

Fiqhi ya Kisunni baada tu ya kuukataa uongozi wa Ahlul-Bait (a.s), ulishika mashiko yake kinyume na yale mashiko ya Ahlul-Bait (a.s). Wao katika masuala ya kifiqhi waliamua kuwafuata masahaba kisha mataabii’na (wafuasi wa masahaba).

Ongezeko la idadi ya Waislamu kutoka nchi mbali mbali, lilisababisha kupatikana kwa maswali mengi mapya ya kifiqi, jambo ambalo kutokana na kule Waislamu kuzifungua au kuziingia nchi mbali mbali, kwa nia ya kutaka kuusambaza utamaduni wa Kiislamu na kuueneza ustaarabu huo ndani ya nchi hizo. Hayo yalitokea mwanzoni mwa karne ya pili Hijiria hadi mwanzoni mwa karne ya nne, matokeo hayo ya ndani ya kipindi hicho, yaliiwivisha fiqhi ya wafuasi wa madhehebu ya Ahlu-Sunna kisawa sawa, na matunda yake yakawa ni kuzaliwa kwa madhehebu manne ya Kisunni.

Kule fiqhi ya Ahlu-Sunna kuchanua na kuzaa madhehebu mane tofauti, kulisababiswha na haja kubwa ya Waislamu wapya walioingia katika dini hii huku wakiwa na aina mbali mbali ya maswali yenye kuhitajia jawabu. Haja hiyo ya kutaka kupata ufafanuzi wa maswali mbali mbali ya kifiqhi, ilikuwa si jambo tu lenye kuhitajiwa na wale Waislamu wapya, bali pia ilikuwa ni mahitajio ya jamii nzima ya Kiislamu. Lakini pia si jambo lenye kusahaulika kuwa: ujanja wa kisiasa haukukaa nyuma katika kuyakuza na kuyakozesha rangi mahehebu hayo manne ndani ya jamii kwa nia ya kuyaweka nyuma ya mgongo wa jamii, yale madhehebu ya Ahlul-Bait (a.s). Baada ya wanasiasa wa zama hizo kujitenga na mfumo wa kifiqhi wa Ahlul-Bait (a.s), waliamua kulijaza au kuliziba pengo hilo kwa hali moja au nyengine kupitia fiqhi ya Ahlu-Sunna.

Ni muhimu watu waelewe kwamba: Ahlu-Sunna hawakuwa na madhehebu manne tu, bali kulikuwa kuna wengi miongoni mwa wanazuoni wa Kisunni waliokuwa na mitazamo yenye kutafautiana, jambo ambalo liliweza kuzaa zaidi ya hayo madhehebu manne, kwani kila mmoja miongoni mwa wanazuoni hao waliokuwa wakiishi katika vitongoji na miji mbali mbali, walikuwa na wafuasi wao, huku wao wakiwa na aina maalumu ya madhehebu yenye kutofautiana na madhehebu mengine ya Kisunni, na baadhi ya madhebu ya wanazuoni hao ni kama: madhehebu ya Hasan Basriy, madhehebu ya Auzai, madhehebu ya Daudi bin Ali Al-Isfahaniy na madhehebu ya Muhammad bin Jariir Tabariy.[3] Lakini kwa kutokana na masuala ya kisiasa, mwishowe madhehebu yote hayo yakafifia, na madhehebu manne tu ndiyo yakawa yaliokubalika na kutukuzwa.

 

Sababu kuu iliyoyafunga madhehebu ya Ahlu-Aunna katika magehebu manne tu

Kutokana na tofauti nyingi za kifiqhi zilizokuwa zikionekana ndani ya madhehebu mbali mbali ya Ahlu-Aunna, tofauti ambazo zikuwa zikileta aina nyingi za mizozo ndani ya jamii, kwa kule wanajamii kutokuwa makubaliano ya kufuata moja kati ya fikra za wanazuoni waliokuwa ndani ya zama hizo. Jambo hili lilisababisha wanajamii kukubaliana na madhehebu hayo manne ili kuepukana na mizozo mbali mbali, lakini hilo halikuzaliwa na msukumo wa fikra za jamii peke yake, bali pia serikali za zama zile zilichangia kwa kiwango kikubwa katika kulihakikisha suala hilo na kulikubalisha ndani ya jamii. Wanajamii wenyewe hawakuwa na nguvu za kuyakubali madhehebu manne maalumu, bali serikali ndiyo iliyofanya kazi ya kuyaainisha madhehebu hayo na kuyapa kipau mbele zaidi madhehebu fulani ndani ya madhehebu hayo manne. Pia pale dhehebu fulani lilipoweza kujisogeza zaidi serikalini na hatimaye kushika nafasi ya ukadhi, ndiko kulikokuwa kulisukuma zaidi dhehebu hilo katika ukubalikaji wake ndani ya jamii. Kwa mfano: madhehebu ya Hanafia, kwa kutokana na nguvu maalumu pamoja na kuwa na nyenzo walizokuwa nazo wafuasi wa dhehebu hili, kulilifanya dhehebu hili kutanda na kuenea zaidi, kwani dhehebu hili liliweza kuutegemea mgongo wa Abu Yusuf aliyekuwa ni kadhi mkuu serikali ndani ya utawala Abbaasiyya (kizazi cha Bani Abbas) katika kusambaa na kuenea kwake, kwani yeye alikuwa akiheshimika sana ndani ya serikali ya utawala huo, hivyo yeye aliituima nafasi hii katika kuwapa wanazuoni wa madhehebu haya nafasi mbali mbali za ukadhi.[4]

 

Waanzilishi wa madhehebu manne ya Kisunni ni kama ifuatavyo:

1- Nuu’maan bin Thabit (Abu Haniifa) aliye fariki mwaka 150 Hijiria.

2- Maalik bin Aanas aliyefariki mwaka 179 Hijiria.

3- Muhammad bin Idris Shafii’ aliye fariki mwaka 204 Hijiria.

4- Ahmad bin Hanbal aliyefariki mwaka 240 Hijiria.

 

Sababu na namna ya kufungwa mlango wa ijitihadi wa Ahlu-Sunna

Ijitihadi ndio msingi wa kuyadumisha maisha ya Uislamu na ndio kamba madhubuti katika kupatikana mabadiliko mbali mbali ya kimaendeleo ndani ya Uislamu. Kivuli hichi cha ijitihadi ndicho kilichotanda kisawa sawa juu ya jamii ya Kiisalamu ndani ya kipindi cha karne 14, na kuwafanya Waislamu wajitegemee wenyewe na wala wasikopi au kuiga mifumo isiyokuwa ya Kiislamu katika kuzalisha sheria na katiba madhubuti ya kisheria kibinafsi na kijamii.

Suala la ijitihadi kwa upande wa madhehebu ya Ahlu-Sunna, lilikuwa ni suala la kawaida kabisa lililoendelea hadi kufikia mwaka 665 Hijiria, lakini kwa kutokana na sababu maalumu, suala hili likawa ni lenye kupuuzwa, jambo ambalo liliyabakisha madhehebu ya Ahlu-Sunna kubaki nyuma na kudumaa ndani ya madhehebu manne tu, huku madhehebu mengine miongoni mwao yakawa ni yenye kufifia na kuporomoka, jambo ambalo lilisababisha nafasi zote zile muhimu za ndani ya jamii, kama vile kusalisha sala za Ijumaa, ukadhi na mengineyo kushikwa na wanazuoni au wafuasi wa mdhehebu manne hayo tuliyoyataja hapo mwanzo.[5] Ama sababu iliyosababisha kufungwa kwa mlango wa ijitihadi, ni kama ifuatavyo:[6]

1- upendeleo sugu wa kimadhehebu

Kule wafuasi wa madhehebu mbali mbali mara nyingi kuwa wana aina maalumu ya upendeleo juu ya kiongozi wao, jambo ambalo huwafanya wao kuwa sugu katika kuto ridhika na kutozivumilia fikra na maoni ya wanazuoni wengine, ndilo lililosababishia wao kuzihesabu fikra na maoni ya wengine kuwa ni batili, na kuto kuwa tayari kuyasikiliza na kuyajadili kielimu na kiakili mawazo na fikra za wengine. Mmoja kati ya wanachuoni wa madhehebu ya Kishia kuhusiana na suala hili amesema: (hisia za aina kama hiyo, zilikuwa ndiyo moja ya sababu zilizosababisha kufungwa kwa mlango wa ijitihadi ndani ya madhehebu ya Kisunni, hisia ambazo pia zilikaribia kuyazorotesha madhehebu ya Kishia, hata kukaribia kuufunga mlango wa ijitihadi ndani ya masdhehebu yetu ya Kishia. Na kile kilichoweza kutuokoa sisi na fitna hii, ni ushupavu wa mmoja kati ya wanazuoni wetu wakuu. Lakini baada ya viongozi wa madhehebu manne ya kifiqhi ya Ahlu-Sunna kufariki na kuziacha jamii zao na aina kama hizi za hisia, hisia hizo ziliweza kuchukuwa nafasi yake ndani ya jamii ya Kisunni na ndani ya madhehebu yao manne, jambo ambalo lilisababisha kila kundi moja kujihisi kuwa ni bora zaidi, na hatimae kila mmoja kujivuna kwa fiqhi yake na kuto vumilia kuwaona wengeni ndani ya uwanja wa ijitihadi wakitoa aina nyengine za fatwa ziendazo kinyume na zile zao wao au za viongozi wao).[7]

 

2- msokotano uliosababishwa na fatwa za makadhi:

Mara nyingi ndani ya jamii kulikuwa kukionekana kuwepo kwa tofauti za fatwa zilizokuwa zikitolewa na makadhi kutoka miji mbali mbali au mahakama mbali mbali, jambo ambalo lilikuwa likisababisha kupatikana kwa mizozo ndani ya jamii, kwani pale kadhi fulani ambaye ni mujtahidi alipokuwa akitoa hukumu fulani, yeye alikuwa akitegea ijitihadi yake katika uwaji wake wa hukumu hiyo, kwa hiyo wale ambo waliokuwa ni wafuasi wa madhehebu mengine, walikuwa wakilalamika kutokana na fatwa na hukumu hiyo. Hapo jamii ikaingia matatizoni kwa kule kila mahakama kutoa aina tofauti ya hukumu juu ya suala fulani. Hali hiyo ilizisababisha serikali kuwalazimisha makadhi wahukumu kupitia moja kati zile hukumu za madhehebu manne tu, na kuto yapindukia madhehebu hayo katika utoaji wao wa hukumu.

3- sababu za kisiasa:

Lililosemwa kuhusiana na hili ni kwamba: (kinacho onekana ni kwamba: mifumo mbali mbali ya kisiasa ya zama zile, ilikuwa ikikhofu aina mbali mbali za miinuko ya kielimu na kifikra kutoka ndani ya vyuo mbali mbali vya kidini. Hii ni kwa kutokana na viongozi wa kisiasa kufahamu kuwa: ndani ya zama mbali mbali, viongozi na wanazuoni wa kidini ndiwo waliokuwa wakiwaamsha watu kifikra na kuwatanabahisha wanajamii wao kielimu, ili waweze kuepukana na aina mbali mbali za uzushi zinazoletwa na viongozi wa serikali dhalimu. Nao pia walikuwa tayari wameshaona hatua mbali mbali zilizochukuliwa na wanadini katika kuuokoa Uislamu, kupitia njia ya uboresha wa jamii kwa kule wao kuzifanyia kazi fikra za Kiislamu ndani ya jamii zao, jambo ambalo lilikuwa likipingana na matamanio potofu ya viongozi dhalimu ndani ya jamii hizo).[8] Pia tusisahau kuwa serikali hizo hazikuwanyima wao aina zote za ijitihadi, bali bado wao waliweza kufanya ijitihadi ndani ya nyanja maalumu kupitia moja kati ya mifumo na misingi maalumu ya madhehebu manne ya Kisunni, kwa hiyo mwanachuoni wa dhehebu fulani alikuwa na ruhusa ya ijitihadi ndani ya dhehebu lake kwa kupitia misingi na mifumo iyendayo sawa na dhehebu hilo kwa ajili ya kutoa hukumu fulani, lakini yeye hakuwa na ruhusa ya kufanya ijitihadi moja kwa moja ndani ya madhehebu hayo manne au nje ya madhehebu hayo. Hii ni baada ya madhehebu ya Ahulu-Sunna kufungwa ndani ya mabano au mfungo wa madhehebu manne tu.

 

 

Pambazuko jipya la Ahlu-Sunna la kuelekea kwenye uhuru wa ijitihadi

Ndani ya miaka ya hivi karibuni kumeanza kusikika mnong’ono ndani ya jamii za wanazuoni wa Ahlu-Sunna kuhusiana na kufunguliwa tena mlango wa ijitihadi.[9] Mnong’ono huu ni wenye kutowa mawazo mapya nayo ni kwamba: mwanachuoni awe ni huru katika kufanya ijitihadi, yaani fikra za ijitihadi zipanuliwe zaidi, na mwanazuoni asijifunge na dhehebu moja tu la Kisunni katika kufanya ijitihadi, bali yeye azitanue na kuzikunjua mbawa za fikra za ijitihadi zake ndani ya madhehebu yote manne ya Kisunni. Hii inatokana na wao kujihisi kuwa ni wenye kukumbwa na maswali mbali mbali yanayozaliwa kila dakika kutoka katika ulimwengu wa maeneleo na teknolojia.

Leo kuna wengi miongoni mwa wafuasi wa madhehebu ya Kisunni wenye kujiuliza: ni kwa nini wao wawe ni wafuasi wa fiqhi fulani iliyoandkwa na mwanachuoni wa zama za kale, mwanazuoni ambaye hakuishi ndani ya zama zetu, na wala yeye hakuelewa hali ya maisha ya watu wa hivi sasa?

Pia wao huwa wanakumbwa na swali lisemalo: iwapo kumfuata mmoja kati ya wanachuoni wa madhehebu manne ya Kisunni katika matendo yetu ya ibada ni wajibu na ni lazima, katika hali kama hiyo, je wao wenyewe walikuwa wakimfuata mwanazuoni fulani? Na kama jawabu itakuwa ndio, basi wao walikuwa ni wafuasi wa nani?

Fikra kama hizi ndani ya ulimwengu wa Kisunni, zimepata wafuasi wengi ndani ya zama zetu hizi za leo. Fikra hizi tayari zimeshasimama mbele ya mlango wa ijitihadi huku zikiugonga mlango huo kwa ajili ya kuufungua na kutafuta maendeleo ya dini ndani yake kwa manufaa ya jamii ya Waislamu na walimwengu kwa jumla.

Mwisho wa makala.

Maswali yenye uhusiano na maka hii ndani ya tovuti yetu ni:

Swali la 796 na namba ya swali hili ndani ya tovuti ni (855), jina la swali ni (ijitihadi ndani ya madhehebu ya Kishia).

Swali la 795, namba ya swali kwenye tovuti ni (854) lenye jina (ijitihadi ndani ya Qur-ani na Hadithi).

Sawli la 4932 namba ya swali ndani ya tovuti ni (5182), jina la swali ni (sababu zilizopelekea kupatikana madhehebu mbali mbali).

 


[1] Taarekhul-Fiqhul-Islamiy-wa Adwaarihi, cha Jaa’far Subhani, uk/14, chapa ya Imam Sadiq (a.s), Qum, mwaka 1427 Hijiria.

[2] Rejea rejeo lililopita.

[3] Rejea rejeo lililopita, uk/64.

[4] Al-Salafiyya Baina Ahlu-Sunna-Wal-Imaamiyya, cha Sayyid Muhammad Kuthairiy, uk/107, chapa ya Ghadir, Beirut, mwaka 1418 Hijiria.

[5] Rahnemaye Haqiiqat, cha Jaa’far Subhaaniy, uk/577, chapa ya Mash-a’r, Tehran, mwaka 1387 Hijiria.

[6] Haya, tumeyatoa ndani ya kitabu: (Taariikhul_fiqhhul-Islaamiy-wa- Adwaarihi), mlangu wa (Asbaabu Ghalqi Baabul-Ijtihaadi).

[7] Shie Shenaasiy wa Paasokh be Shubuhaat, cha Ali Asghar Ridhwaniy, juz/, uk/615, chapa ya Mash-a’r, Tehran, mwaka 1384 Shamsia.

[8] Rejea kitabu kilicho pita.

[9] Baadhi ya wanatafakuri wa Madhehebu ya Kisunni wameonekana kuandika makala mbali mbali kuhusiana na mada hii, na miongoni mwao ni Muhammad Ali Saayis (محمد علی سایس) na Ali Mansuur Al-Misriy (علی منصور المصری). Rejea kitabu kiitwacho: Taarikhul-Fqhil-Islaamiy-wa-Adwaarihi (تاریخ الفقه الاسلامی و ادواره), uk/100.

 

TARJAMA YA JAWABU KATIKA LUGHA NYENGINE
MAONI
Idadi ya maoni 0
Tafadhali ingiza thamani
mfano : Yourname@YourDomane.ext
Tafadhali ingiza thamani
<< Niburute.
Tafadhali ingiza kiasi sahihi ya usalama Kanuni

MPANGILIO WA KIMAUDHUI

MASWALI KIHOLELA

YALIYOSOMWA ZAIDI