Please Wait
9593
Fani ya Fiqhi iliyo katika nyanja za juu (iliyobobea), huwa inampa mtu uwezo maalumu wa kuzivua na kuziopoa hukumu kuu za kisheria kutoka katika machimbuko yake, ambayo miongoni mwayo ni zile ibara za Qur-ani na Hadithi takatifu, na jambo hilo (kuwa na uwezo wa kuziopoa hukumu) ni lenye umuhimu katika nyanja zote, iwe ni kwa ajili kutoa fatwa, kutoa hukumu mbali mbali za kijamii au kwa ajili ya kuiongoza jamii kisiasa, wadhifa ambao huwa ni jukumu lililoko juu ya shingao ya kiongozi mkuu wa dini. Na kila moja kati ya hayo tuliyoyataja, huwa yanaambatana na upande maalumu wa fani ya Fiqhi, lakini kila mmoja kati wale wataalamu wa mambo hayo huwa wanaitwa ni wanafiqhi au (mafuqahaa), neno ambalo linatokana na lugha ya Kiarabu. Kazi muhimu kwa yule mwanachuoni (mwanafiqhi) anayetaka kutoa fatwa, ni kuzimiliki hukumu maalumu za kisheria kwa kupitia dalili zilizoegemea kwenye machibuko ya sheria hizo, kisha kuzitangaza hukumu hizo kwa wafuasi wake wanamkubali na kumthamini, na wafuasi wake ni wale watu wasiokuwa na ujuzi tosha juu ya masuala mbali mbali ya dini, kwa kuwa ni wajibu wa kila mjinga kumtegemea mweruvu, ama katika yale masuala ambayo mtu atakuwa na ujizi nayo, basi huwa hakuna haja ya kumtafuta wa kumshika mkono katika mambo hayo na kumpa msaada. Ama kuhusiana na suala la kuandama kwa mwezi, suala hili huwa si lenye kutaka ujuzi wa kielimu, bali ni suala lenye kuhitajia tu uangalifu maalumu wa kuuangalia mwezi au kuhakikisha kuwa mwezi umeandama, kwa hiyo suala hili linamuhusu kila mmoja mwenye macho ya kuuangalia mwezi, isipokuwa tu wakati mwengine kunaweza kukapatikana baadhi ya matatizo ya hali ya hewa, jambo ambalo huwa ni chagizo kwa mtu wa kawaida aseye na vifaa.
Wadhifa muhimu wa kiongozi mkuu wa dini (mwanafiqhi / kadhi), ni kutowa fatwa mbali mbali pamoja na kuiongoza jamii kwa kupitia misingi imara ya dini, na ni wajibu wa kila mmoja kuitii serikali ya kiongozi huyo. Hivyo basi ingawaje suala la kuonekana kwa mwezi si jukumu maalumu la kiongozi huyo tu, lakini kwa kutokana na kuwa jamii ni yenye kumtegemea yeye katika masuala mbali mbali ya kijamii, hali ambayo inamfanya yeye awe ndiye muhusika mkuu wa kuutangaza mwezi.
Viongozi wa dini wakati mmoja huwa ni wenye kudhihiri katika jamii wakiwa ni kama watibabu wenye kutoa huduma maalumu za kijamii, na wakati mwengine hudhihiri wakiwa ni viongozi wakuu wa jamii hizo wenye kutoa huduma zote za kijamii pamoja na kisiasa kwa njia moja au nyengine. Mtume wetu (s.a.w.w) alikuwa amebeba aina zote mbili za nyadhifa, Yeye (s.a.w.w) alikuwa akitoa fatwa makhsusi za kidini zenye kumuelekea mtu mmoja mmoja, na kwa upande wa pili alikuwa ni kiongozi wa jamii nzima mwenye kutoa fatwa za kisiasa na kijamii, kama vile fatwa za jihadi na suluhu mbali mbali.[1] Na wajibu kama huo haukuwa ni wa Mtume (s.a.w.w) peke yake, bali ulikuwa na wa kila imam aliyekuja kwa niaba ya Yake (s.a.w.w).
Katika zama ambazo uma umekuwa uko mbali na imamu, watu wamekuwa wakiwarudia mafuqahaa kwa ajili ya kuzitambua huku maalumu za kisheria zenye kuwafafanulia aina mbali mbali za namna ya utekelezaji wa ibada zao za kila siku, haidhuru huwa kuna baadhi ya usumbufu unaopatikana kuhusiana na masuala kama hayo, lakini bado wanafiqhi hawatofautiani sana katika utoaji wa fatwa kuhusiana na mambo kamo hayo, jambo ambalo huwa ni lenye kuirahisishia jamii kuzifuata fatwa hizo bila ya utata mkumbwa na mgongano ndani ya jamii. Tatizo kubwa linaloikabili jamii katika zama ambazo imam anakuwa yuko nje ya jamii au anapotoweka, ni kule jamii kukosa fatwa za kisiasa pamoja na fatwa za kimahakama, baadhi ya watu wanafikiri kuwa aina hizi za fatwa ni sawa na zile fatwa za kaida za kifiqhi, kiasi ya kwamba yawezekana mtu kumfuata kiongozi yeyote yule wa kidini na kuchukuwa fatwa za mambo kama hayo kutoka kwake.
Basi je hivi kuna uwiano wowote ule baina ya masuala ya kuandama kwa mwezi au kuitangaza idi na baina ya masuala mengine ya kifiqhi kama vile: masula ya sala na hukumu zake za kifiqhi?
Jawabu ya swala hili utaipata katika ufafanuzi ufuatao:
1- nyadhifa za mwanafhi mwenye sifa za kufuatwa:
Nyadhifa muhimu za mwanafiqhi ni:
Kuimiliki fani ya fiqhi na kutoa fatwa pamoja na kuupa nasaha uma.[2]
2- nyadhifa za kiongozi mkuu wa kidini (mwanafiqhi / kadhi):
Wadhifa mkuu wa kiongozi huyu, ukiongezea na ule wadhifa wa mwanafiqhi wa kawaida, ni kuiongoza jamii kwa kupitia vipimo na misingi ya Kiislamu,[3] na kiongozi huyo anaweza kuiongoza jamii kwa kutokana na hali ya jamii yenyewe ilivyo, vile vile ni wajibu wa kila mmoja kuzitii amri zote za serikali ya kiongozi huyo.[4]
Ni muhimu kufahamu kuwa: kiongozi wa kidini anaweza kuitangaza hali maalumu katika nchi au kukataza kitu fulani au pia kweka sheria maalumu kuhusiana na jambo fulani kwa kutokana na hali na zama zilivyo, na kufanya hivyo kunazingatia masuala ya kisiasa na hali nzima ya kuihifadhi jamii ya kiislamu kutokana na matatizo mbali mbali ya kijamii na kisiasa. Na kwa kutokana na kutafuta usalama wa kutopatikana msongomano ndani ya jamii, fatwa na sheria hizo zinazatakiwa kutolea na kiongozi mkuu wa kidini wa jamii hiyo. Lakini kwenye masula ya kawaida, huwa hakuna tatizo la wanazuoni kutoa mitazamo na fatwa tofauti, kwani kufanya hivyo huwa hakuwezi kuleta mvurugiko ndani ya jamii.
Kuutangaza mwezi:
Saahibul-Jawahiri ni mmoja kati watu wenye kuunga mkono mtazamo wa utawala wa kiongozi mkuu wa kidini katika nyanja zote, yeye anaona kuwa: suala la kuutangaza mwezi ni wadhifa tu wa kiongozi mkuu wa Kiislamu.[5]
Katika fani ya Fiqhi, suala la kuonekana kwa mwezi halionekani kuwa ni lenye kukubalika na kuthibitika kwa kauli ya mwanachuoni fulani wa ndani ya jamii, bali suala la kuthibiti kwa mwezi ndani ya jamii fulani limeegemezwa kwenye shingo ya kiongozi mkuu wa dini.[6]
Kwa hiyo ingawaje suala la kuandama kwa mwezi si suala maalumu lenye kuwahusu wanavyuoni peke yao, lakini kwa upande mmoja ni suala la kijamii linaloifunganisha jamii katika mtindo mmoja, na muhusika hasa wa kuisaidia na kuiongoza jamii kijamii na kisiasa ni kiongozi mkuu wa Kiislamu, basi yeye ndiye atakaye kuwa muhusika mkuu wa suala hilo.
Jawabu kutoka kwa mwanachuoni Ayatulla Mahdiy Hadawiy Tehraniy (Mungu amhifadhi):
Kuutangaza mwezi ni jukumu na wadhifa wa kiongozi mkuu wa Kiislamu.
[1] Wilayat wa diyaanat, cha Mahdiy Hadawiy Tehraniy, uk/138, chapa ya tano ya Muaseseye Farhangiy Khoone Khirad ya mwaka 1389 Shamsia.
[2] Rejea kitabu kilicho pita.
[3] Wilayat wa diyaanat, cha Mahdiy Hadawiy Tehraniy, uk/141.
[4] Wilayat wa diyaanat, cha Mahdiy Hadawiy Tehraniy, uk/121 hadi 122. Sherehe ya Imam Khomeiniy ya kitabu Tawdhuhul-masaail, juz/1, uk/35, suala la 55, uk/36, suala la62.
[5] Jawahirul-kalaam, juz/40, uk/100.
[6] Kitabu Siratun-najaat chenye sherhe ndani yake, uk/193 na swali na jawabu, uk/120. Sherehe ya Imam Khomeiniy ya kitabu Tawdhuhul-masaail, juz/1, uk/959-961, chini ya suala la 1730nasuala la1731.