advanced Search
KAGUA
11879
Tarehe ya kuingizwa: 2012/05/21
Summary Maswali
kwa mtazamao wa Kiislamu, mwanaadamu ni kiumbe gani?
SWALI
kwa mtazamao wa Kiislamu, mwanaadamu ni kiumbe gani?
MUKHTASARI WA JAWABU

Kwa mtazamo wa Qur-ani, mwanaadamu ni kiumbe aliyebeba sifa mbili tofauti za kimaumbile, moja ni ile inayotokana na maumbile aliyopewa tokea mwanzo kutoka kwa Mola wake, nayo ni maumbile ya kiroho, na ya pili inatokana na maumbile ya kiwiliwili alichonacho. Maumbile asili ya kiroho (kifitra), huwa ni yenye kiu ya kujichumia sifa njema na humlingania mja huyo kutenda mema, lakini upande ule wa kiwiliwili huwa ni wenye kumvuta katika masuala ya kidunia au masuala yenye kufungamana na mwili wake, pia humuamrisha kuelekea katika maovu kwa kule kumtaka yeye akifuate kila anachotamani kukifanya. Tabia mbili za kimaumbile alizonazo mwanaadamu, huyafanya maisha ya mwanaadamu siku zote kuwa ni uwanja wa mapambano, hii ni kutokana na kuwepo mvutano baina ya pande mbili hizo. Kwa mtazamo wa Qurani mtu aliyeuendekeza mwili wake na kufanya kila analolitamani kwa ajili ya matakwa ya mwili huo, ni mtu aliyepotea njia, lakini iwapo mwanaadamu atashikamana na matakwa ya kiroho yanayomuhimiza kuzipalilia tabia njema na kujivunia sifa za ukamilifu, huyo atakua katika njia ya uongofu, naye atahisabiwa kuwa ameshikamana na haki kisawasawa. Kwa mtazamo wa Qur-ani, mwanaadamu kwa mara ya kwanza kabisa pale anapoukita mguu wake duniani, huwa ni kiumbe anayeikanyaga dunia bila ya kuwa na elimu wala mawazo ya aina yeyote, likini binaadamu huyu ndani ya maumbile yake huwa amebeba mche mchanga wa muongozo safi wa kimaumbile aliyotoka nao kwa Mola wake, na wakati huo huo ana yale maumbile ya kiwiliwili yanayomvuta yeye kuelekea katika kuutii mwili huo, nao pia ni mche au mbegu ya kimaumbile ambayo yaweza kukua na kumletea athari maalumu. Baada ya muda mchache tu baada ya mwanaadamu kuingia ulimwenguni humu, huanza kupata elimu kwa kupitia misingi mbali mbali aliyonayo, na kwa kupitia maumbile ya kiroho aliyonayo hujipatia miongozo iliyo safi itakayoshika sukani ya kumuongoza yeye katika njia sahihi pale ataposhikamana nayo, na huo ndio mtazamo wa Qur-ani kuhusiana na mwanaadamu, hivyo basi kwa mtazamo huo, wanaadamu wote ni wenye aina moja ya kimaumbile, na ni wenye kiini kimoja cha ubinaadamu, kiini ambacho huwa ndio msingi mkuu wa haki za kibinaadamu ndani ya Uislamu.

JAWABU KWA UFAFANUZI

Tunapolizungumzia suala la kumtafiti na kumtambua mwanaadamu kwa kupitia darubini ya Kiislamu, huwa tunakusudia kutafuta picha nzima inayotolewa na Uislamu kuhusiana na kiumbe huyo.

 

Kuhusiana na suala la uhakika wa mwanaadamu, kuna aina mbili za mitazamo inayoweza kuzungumziwa suala hili katika njia ya utoaji wa ufafanuzi katika kuukamilisha utafiti juu ya mwanaadamu. Moja kati ya mitazamo hiyo miwili, ni ule mtazamo usemao kuwa: wanaadamu wote ni wenye kiini kimoja cha ubinaadamu kisicho tofautiana kutoka mwanaadamu mmoja kwenda mwengine, na tofauti zinazoonekana kati yao kama vile, tamaduni, rangi, lugha na mengineyo, vitu hivi huwa havina mchango wowote ule katika kuthibitika kwa ubinaadamu wa mtu fulani, bali yote hayo huwa ni kava ya ya nje ya kila mmoja wetu inayomtofautisha yeye kutokana na wengine wasiyokuwa yeye, na upande wa pili kuna mtazamo unaoona kuwa: mila, tamaduni, na mengineyo, huwa vinachangia katika uthibitikaji wa ubinaadamu, na mtazamo huu unawaona wanaadamu kuwa ni wenye kutofautiana katika uhakika wao wa kibinaadamu.

 

Baina ya mitazamo miwili hii, mtazamo wa kwanzo ndio uliokubaliwa na wanachuoni mbali mbali wa kidini na Kifalsafa, ingawaje katika ufafanuzi wa kulifafanua suala hilo, kila mmoja hushika njia yake kwa jinsi ya fani na elimu yake ilivyo.

Vile vile kuna baadhi ya Wanafalsafa wa zama za hivi sasa wanaouwafiki mtazamo wa pili, wao basi wanaona kuwa: tofauti za kitamaduni huwa ni sababu za kutofautiana uwanaadamu wa watu mbali mbali. Hivyo basi kuna Wanafalsafa wenye kuyatumia maneno maalumu kama vile: mwanaadamu wa kale (mshamba) na mwanaadamu wa kileo (mstaarabu), huyatumia maneno kama hayo kwa ajili ya kuonesha tofauti za kibinaadamu zilizoko baina yao.

 

Waandishi mbali mbali wanapoligusia sula la uwanaadamu na kutaka kuthibitisha kuwepo kwa tofauti za kibinaadamu miongoni mwao, huwa wanakusudia kuashiria lile tokeo la kitarehe lililotokea katika zama za (Renaissance).[1]  Lililo kweli ni kwamba, mabadiliko ya kitamaduni na kisiasa yanayotokea katika zama tofauti, huwa si yenye kuwabadilisha na kuwatofautisha wanaadamu mbali mbali katika ubinaadamu wao, bali kinachotokea katika mapinduzi ya kimaendeleo ndani ya zama mbali mbali, huwa ni sababu tu zinazoyageuza maisha ya wanaadamu kutoka katika picha moja kwenda nyengine, na sio kuwabadilisha wao kidhati na kuwapa dhati mpya (kiini kipya).

 

Uislamu unawaona watu wote kuwa ni sawa kiubinaadamu, ingawaje wao huwa ni wenye kutofautiana kitamaduni, kiitikadi, kirangi na kikabila, lakini bado wao kireja reja na kiujumla ni wenye aina moja ya ubinaadamu, na wao si wenye kutofautiana katika hilo. Wanaadamu kuwa ni wamoja katika ubinaadamu wao, ni suala lenye kusadikiwa na Qur-ani, Falsafa pamoja na kusadikiwa na kila mwenye upeo wa kielimu, na hata elimu ya Sayansi ni yenye kulisadikisha jambo hilo.

Kwa mtazamo wa Kiislamu ni kwamba wanaadamu wote wameumbwa katika maumbile mawili, nayo ni ya kiroho nay a kiwili wili, na iwapo mwanaadamu atayatunza vyema maumbile yake ya kiroho na kuyakuza, hapo yeye ataweza kupata maendeleo kamili ya kiroho, lakini iwapo atayapuuza maumbile yake ya kiroho na kuyakuza yale maumbile yake ya kiwili wili, hapo yeye ataboreka kidunia na kunyongonyea kiroho na kiubinaadamu.

 

Qur-ani mara kwa mara humzungumzia mwanaadamu kwa sifa mbali mbali, mara nyengine humzungumzia kwa sifa njema na mara nyengine kwa sifa mbaya. Hivyo basi iwapo utaiangalia vyema Qurani, utakuta ndani yake zile Aya zinazomsifu mwanaadamu kwa kule yeye kuumbwa kwa  umbile bora litokalo kwa mola wake, kama vile Aya ifuatayo isemavyo:

«فطرت‏الله التى فطرالناس عليها» maana yake ni kwamba: (Maumbile aliyoumbwa nayo mwanaadamu, ni maumbile yatokayo kwa Alla).[2] Na kwa upande wa pili kuna zile Aya zinazomsifu yeye kwa sifa mbaya, na miongoni mwazo ni ile Aya isemayo:  «خلق الانسان هلوعاً» maana yake ni kwamba: (Kwa hakika mwanaadamu ameubwa huku akiwa na sifa ya kutokuwa na subira).[3]

 

 

Kumzungumzia mwanaadamu kwa sifa njema au mbaya hakumaanishi kuwa mwanaadamu tayari ameshakuwa na sifa hizo, au yeye huzaliwa huku akiwa yeye ameshapewa aina fulani za sifa mbaya au njema, bali kinachokusudiwa kuelezewa ni kwamba, mwanaadamu ameumbwa huku akiwa yeye ana aina mbili za misingi, msingi wa kusimamisha jengo la uovu na msingi wa kusimamisha jengo la wema, na hiyo ndiyo maana ya mwanaadamu kuwa na uhuru kamili wa kimaumbile. Ukweli huu huwa wazi mbele ya kila mwenye kuisoma Qur-ani kwa makini kwani kama tulivyosema hapo mwanzo kuwa Qur-ani imemsifu mwanaadamu kwa sifa mbali mbali kama vile, kutovumilia tabu na kutoshukuru, na kwa mara nyengine humpa sifa nzuri kama vile, kiumbe bora, khalifa wa Mola juu ya ardhi na mengineyo. Qur-ani haikusudii kutuambia kuwa, mwanaadamu huzaliwa huku akiwa na sifa fulani, bali kinachokusudiwa hasa ni kuielezea hali halisi ya maumbile ya mwanaadamu yalivyo, na Qurani ikiashiria ukweli huu imesema:

«والله اخرجكم من بطون امهاتكم لاتعلمون شيئاً»maana yake ni kwamba: (Na Mola wenu amekutoeni kutoka katika matumbo ya mama zenu mkiwa hamtambui kitu).[4]

kwani ndani ya uhakika wa kila mtu huwa kuna mbegu zilizoatikwa ndani ya maumbile yake, naye huwa ana hiyari kamili katika ukuzaji na utiliaji wake wa mbolea, basi yeye mwenyewe ana uhuru kamili wa kuikuza mbegu ya uovu au mbegu ya wema iliyoatikwa kimaumbile ndani ya maumbile yake.

 


[1] Renaissance ni jina la mapinduzi ya kuleta mageuzi ya kistaarabu pamoja na usawazishaji wa dini ya Kikristo yayiyofanyika ndani ya karne zilizopita.

[2] Suratu Ruum, Aya ya 30.

[3] Suratul-Maa’rij, Aya ya 19.

[4] Suratun-Nahli, Aya ya 78.

 

TARJAMA YA JAWABU KATIKA LUGHA NYENGINE
MAONI
Idadi ya maoni 0
Tafadhali ingiza thamani
mfano : Yourname@YourDomane.ext
Tafadhali ingiza thamani
<< Niburute.
Tafadhali ingiza kiasi sahihi ya usalama Kanuni

MPANGILIO WA KIMAUDHUI

MASWALI KIHOLELA

YALIYOSOMWA ZAIDI