Please Wait
13115
Dini ni chombo maalumu kilichokuja kumkomboa mwanaadamu na kumuongoza katika njia ya mafanikio, hivyo basi ni jambo lisiloingia akilini kuwa chombo hichi kiwe ni chenye kulipa mgongo jambo muhimu linalohitajika ndani ya jamii mbali mbali, kama vile suala la usimamishaji wa serikali. Na kwa upande mwengine ni kwamba, mjengeko na mfumo mzima wa sheria za Kiislamu ni wenye kuhitajia kuwepo kwa serikali madhubuti, na bila ya kuwepo kwa serikali hiyo, Uislamu hautoweza kuishi maisha yake kwa amani bila ya usumbufu.
Mtu anapoivuta picha halisi ya dini ndani ya akili yake, huku akifahamu kuwa dini ndiyo marejeo makuu ya siasa, hapo atapofahamu kuwa kuwepo kwa serikali ni jambo linaloingia akilini bila ya pingamizi yeyote. Wanaadamu wakiwa ni kama wasafiri ndani ya ulimwengu huu, dini huwa ndiyo kiongozi madhubuti kwa ajili ya kuwaongoza njia iliyo salama itayowafikisha salama na kuwaepusha na matatizo wakiwemo ndani ya msafara wao. Kwa kutokana na umuhimu wa kuwepo kwa serikali ndani ya jamii za kibinaadamu, dini huwajibika kuwasimamishia wanajamii wa jamii tofauti serikali itakayoweza kuwatatulia matatizo yao pamoja na kuwarahisishia njia za uongofu. Imam Ridha (a.s) alilibainisha suala la umuhimu wa kuwepo kwa serikali kwa kusema: (mtu hawezi kuona kuwa kuna watu fulani walioishi bila ya kuwa na msimamizi wa mambo yao, kwani mambo yao ya kidini na kidunia ni yenye kuhitajia msimamizi wa kuyasimamia pamoja na kuwapangia mipango maalumu juu ya mambo hayo. Si jambo la hekima kuwa Mola awawache waja wake bila ya kuwa na msimamizi wa mambo yao, hivyo basi elewa kuwa Mola ni mwenye kufahamu kuwa, waja wake hawana budi kuwa na kiongozi atakayeinyanyua jamii yao na kuwaongoza pale wanapohujumiwa, pia kuigawa mali ya jamii baina yao kwa haki, kusimamisha sala ya Ijumaa pamoja na kuupa nguvu mgongo wa jamii yao, vile vile kuwalinda na kuwahifadhi kutokana na maadui zao)[1] mwisho wa kunukuu, na ukiangalia kwa makini utaona kuwa, mfumo na mjengeko kamili wa sheria za Kiislamu unahitajia kuwepo serikali, na Uislamu bila ya kuwepo kwa serikali hauwezi kusimama na kudumu. Imamu Ridha (a.s) alipokuwa akizungumzia suala la kusimamisha sala ya Ijumaa, alifikia kipengele fulani kinachohusiana na masuala ya uongozi akasema: (Angelikuwa Mola hakuwapelekea waja wake kiongozi muaminifu mwenye kuaminika, basi dini ya Mola ingelitoweka, sheria na miongozo yake ingeligeuzwa, uzushi mbali mbali ungeliongezeka, wasio wachamungu wangeliinyosha mikono yao kwenye dini na kuizorotesha, pia wangaliingiza aina mbali mbali za pingamizi ndani ya dini.)[2]
Umuhimu huu uliotajwa katika Hadithi hizi ni wenye kudhihiri zaidi pale sisi tutapoiangalia serikali ya Kiislamu ya Mtume (s.a.w.w) ilivyojengeka huko Madina, na hilo ni jambo lilithibiti mbele ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu, ingawaje kuna baadhi ya watu wanaojaribu kulipinga suala hilo. Miongoni mwa wakanushaji wa jambo hili, ni yule muandishi maarufu wa Kimisri ajulikanaye kwa jina la Ali Abdul-Razaq ndani ya mwaka 1343 Hijiria aliyejaribu kukanusha kuwepo kwa serikali ya Kiislamu iliyosimamishwa na Mtume (s.a.w.w), pale aliposema ndani ya kitabu chake (الاسلام و اصول الحكم),[3] kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni Mtume pekee aliyekuwa hakusimamisha dola,[4] lakini kauli hii ilimsababishia muandishi huyu kuhujumiwa na wanachuoni mbali mbali wa madhehebu ya Kisunni na kuitwa kafiri, yeye aliendelea kuelezea ndani ya kitabu chake kuwa: Mustafa Kemal Atatürk alipingana na utawala wa Kiothamani huko Uturuki, na mwishowe akautangaza utawala wa Kilaiki, lakini wananchi wa Misri ambao walikuwa ni wafuasi na wapenzi ukhalifa, walimchukuwa mfalme Fuadi na kumfanya kuwa ni khalifa wa Waislamu na wakampa utawala. Maelezo haya yanaonesha kuwa mwandishi huyu aliambukizwa fikra za Kimagharibi, naye anaonekana kuyanukuu maneno hayo kutoka kwa baadhi ya Wanafalsafa wa Kimagharibi pamoja na Wanasiasa wa Kilaiki.
Maandiko ya muandishi huyu yalikuwa yakibeba aina mbili za madai:
1- kile alichokijenga Mtume (s.a.w.w) huko Madina hakikuwa ni serikali.
2- kile alichokijenga hakikuwa na uhusiano na dini.
Yeye katika kulithibitisha suala namba moja alitilia mkazo suala hilo kwa kusema: kile alichothibitisha Mtume (s.a.w.w) na kukijenga huko Madini, hakikuwa na aina yeyote ile ya sifa za serikali kama vile serikali inavyojulikana mbele ya kila mmoja wetu. Na alijaribu kulithibitisha suala namba nmbili kwa kusema kuwa: Mtume (s.a.w.w) alikuwa na hadhi kubwa na hadhi yake haimruhusu yeye kujishirikisha na mambo ya Kisiasa.
Katika kuyajibu madai namba moja, inatubidi kuzingatia kuwa: iwapo neno serikali litakuwa na maana tu ya mfumo maalumu wenye sura maalumu, ndipo sisi tunapoweza kuupa mfumo huo jina la serikali, hapo sisi tunakubaliana naye kuwa hakuna hata zama moja zilizowahi kuwa na serikali. Hivyo basi kwanza kabisa inatubidi sisi kupata maana na ufafanuzi madhubuti kuhusiana na neno serikali, maana ambayo itakuwa ni yenye kuzitumbukiza aina na mifumo yote ya serikali mbali mbali katika chungu kimoja.
Neno serikali laweza kupata ufafanuzi na maana kama ifuatavyo:
Serikali ni mkusanyiko wa nguvu maalumu zilizojengwa kwa ajili ya kuiongoza jamii. Maana hii inaingiza ndani yake vitengo vyote vya kisheria vyenye kuongoza, vikiwemo kitengo cha upangaji wa sheria pia kitengo cha usimamishaji wa hukumu mbali mbali.[5]
Kwa msingi huu basi, kile alichokisimamisha Mtume (s.a.w.w) huko Madina kilikuwa ni serika na si kitu chengine, kwani wadhifa wake ulikuwa ni kuisimamia jamii na kuiongoza kwa kupitia nguvu maalumu na misingi maalumu. Na kuhusiana na suala hili kuna vitabu mbali mbali vilivyolielezea suala hilo kibaga unaga!
Ama kuhusiana na kuwa: je ile serikali ya Mtume (s.a.w.w) ilikuwa ni ya kidini au la, inatubidi kuzingatia mambo yafuatayo:
- miongoni mwa sheria za Kiislamu, kuna sheria ambazo haziwezi kutekelezwa bila ya kuwepo serikali ya Kiislamu, na mfano wa sheria hizo ni sheria zinazohisiana na makosa ya jinai, au sheria za kimahakama, au pia sheria zinazohusiana na mali za Kiislamu.
- Ingelikua suala la siasa ni lenye kwenda kinyume na heshima za unabii, basi vipi Mtume (s.a.w.w) alikuwa akipoteza muda mwingi katika kulishughulikia suala hilo? Iwapo mtu atajibu kuwa Mtume (s.a.w.w) alifanya hivyo kwa kutaka kufaulu katika ulingano wake, jawabu hii itaonesha fungamano madhubuti lililopo baina ya siasa na dini, lakini pia hiyo haitokuwa ni jawabu tosha, kwani yeye alikuwa akilishighulikia mwenyewe suala hilo la kusimamisha dola, na ingelikuwa jambo hilo halina umuhimu, basi angaliweza kuliwakilisha kwa mtu mwengine ili alishughulikie kuliko yeye kupoteza muda wake.
Kwa vyovyote vile yale aliyoyataja muandishi Ali Abul-Razaq katika miaka 70 iliyopita ambayo hukaririwa kwa namna moja au nyengine katika zama zetu za leo, hayatojibika vizuri mpaka pale sisi tutapoliendea shina la fitna hizi huko Umagharibini, na baada ya kufahamu asili ya tatizo lilivyo pamoja na kuzisoma fikra za Kifalsafa za Wanafalsafa wa Kimagharibi na kuutambua Ukristo vilivyo, hapo ndipo tutapoweza kutoa tiba halisi ya tatizo hili.
Kwa ajili ya kupata faida zaidi unaweza kutalii:
Wilayat wa diyaanat cha Ayatullahi Mahdi Hadawiy Theraniy, kilichopigwa chapa na Muaseseye farhangiy khoneye khirad, Qum Iran, mwaka 1380 Shamsia.
[1] Rejea kitabu Biharul-Anwaar cha Majlisi, juz/6, uk/60.
[2] Rejea kitabu kilichopita.
[3] Islam wa rishehaye hukumat.
[4] Ali Abdul-Razaq katika kitabu (Al-Islam wa usulil-hukmu), uk/80.
[5] Basi serikali lina maana ya neno Government.