Please Wait
14723
- Shiriki
Wajukuu hawa wawili wa Mtume (s.a.w.w) ni mabwana wenye utukufu juu ya vijana wote Peponi, haidhuru kuwa ndani ya Pepo watu wote watakuwa katika hali moja ya ujana, ama wao (Imamu Hasan na Husein (a.s)) ndio watakaong’ara zaidi katika wale vijana waliouwawa katika njia ya Mola, au wale waliofariki katika umri wa ujana wao, na hilo si lenye kuupiku ule utukufu wa Mitume na Mawalii wengine wa Mwenye Ezi Mungu juu ya watu wa Peponi.
Na la pili lenye kutaka mazingatio katika Hadithi yenye kuzungumzia suala hili ni kwamba: Riwaya hii imewatukuza wajukuu hawa wawili wa Mtume (s.a.w.w) juu ya watu wa kawaida Peponi, na wala haikusemwa kuwa Wao (a.s) watakuwa ni watukufu hata kuwapindukia Maimamu pamoja na Mitume (a.s).
Mitume na Maimamu (a.s), ni watukufu kuliko wote miongoni mwa watu wa Peponi, kwa hiyo wote kwa ujumla akiwemo Imamu Hasan na Husein (a.s), ni wenye utukufu zaidi kuliko wale watu wengine wa Peponi, lakini tusisahau kuwa: kila mmoja miongoni mwa Mitume, Maimamu na Mawalii wa Mwenye Ezi Mungu, ni mwenye sifa maalumu inayompambanua na wengine. Pale basi Fatima (a.s) anaposifika kwa sifa ya kuwa Yeye ni bibi mtukufu kuliko wanawake wote wa Peponi, au pale Mmoja wa Maimamu (a.s), anapopewa sifa ya kuitwa bwana wa wenye kusujudu, huwa haimaanishi kuwa Fatima (a.s) amewapita mawalii wote kwa utukufu, na wala Yule Imamu aliyeitwa bwana wa wenye kusujudu, huwa kauli hiyo haimaanishi kuwa Yeye (a.s) ni bwana tu wa wenye kusujudu, na si bwana wa wale wasiosujudu, bali kila mmoja miongoni mwao huwa ameshikama na jambo au sifa njema maalumu yenye kumsababishia yeye kupata sifa ya aina fulani.
Kwa hiyo huwa si swali la kimantiki mtu kuuliza kuwa: je hivi huyu bwana wa kusujudu amempita hata Mtume kwa kusujudu? Au kuuliza: je ni yeye tu ndiye aliyepata utukufu kwa kutokana na kusujudu sana, na hakuna mwengine aliyepata utukufu na sifa hiyo zaidi yake?!
Kwa hivyo hakutokuwa na tatizo katika kuwasifu Imamu Hasan na Husein (a.s), na kuwaita kuwa wao ni mabwana wa vijana wa Peponi, na hii inatokana na kule Wao (a.s) kuutoa ujana wao muhanga kwa ajili ya Uislamu, na wala hakukuwepo vijana waliopata heshima zaidi yao ndani ya zama za Mtume (s.a.w.w) na baada ya zama hizo, na pia hakukuwepo vijana waliowazidi Wao (a.s) kwa ucha-Mungu. Basi hakuna kosa kuwaita Wao (a.s) ni mabwana wa vijana wa Peponi, kwani wao si mabwana tu wa vijana, bali ni mabwana wa watu mbali mbali watakaokuwa ndani ya Pepo ya Mola Mtakatifu.
Ili kuwatoa watu mashakani kuhusiana na hilo, sisi tumeamua kulisimamishia dalili swali lako kupitia Riwaya mbili zifuatazo:
- (قَالَ أَبُو عَبْدِ اللَّهِ ع زُورُوا قَبْرَ الْحُسَيْنِ ع وَ لَا تَجْفُوهُ فَإِنَّهُ سَيِّدُ شَبَابِ أَهْلِ الْجَنَّةِ مِنَ الْخَلْقِ وَ سَيِّدُ شَبَابِ الشُّهَدَاء.)[1]
Maana yake ni kwamba: (Imamu Sadiq (a.s) amesema: lizuruni kaburi la Husein (a.s) na wala msikate mguu (msiache kulizuru), kwani Yeye ni bwana wa vijana wa Peponi na ni bwana wa wahanga, (vijana waliojitoa muhanga kwa ajili ya Uislamu.)
Riwaya hii hakumsfu tu Imamu Husein (a.s) kwa kumuita ni bwana wa wahanga, bali imesema kuwa Yeye (a.s) ni bwana wa wahanga vijana, nyongeza ya neno (vijana), inaashiria aina maalumu ya utukufu kwa wahanga vijana, na wala neno hilo halikutumika kiholela ndani ya Riwaya hii.
- (عن علي ع قال قال رسول الله ص أتاني ملك فقال يا محمد إن الله تعالى يقول لك إني قد أمرت شجرة طوبى أن تحمل الدر و الياقوت و المرجان و أن تنثره على من قضى عقد نكاح فاطمة من الملائكة و الحور العين و قد سر بذلك سائر أهل السماوات و إنه سيولد بينهما ولدان سيدان في الدنيا و سيسودان على كهول أهل الجنة و شبابها و قد تزين أهل الجنة لذلك فاقرر عينا يا محمد فإنك سيد الأولين و الآخرين.)[2]
Maana yeke ni kwamba: (Imamu (a.s) Mtume (s.a.w.w) akisema: amenijia Malaika akanambia: Ewe Muhammad…..kisha watazaliwa watoto wawili (Hasan na Husein (a.s)) nao watakuwa ni mabwana na watukufu hapa ulimwenguni, kisha Wao (a.s) ndiwo watakaokuwa ni pambo la wakongwe na vijana wa Peponi…..)
Ndani ya Riwaya hii kumetajwa matabaka mawili ya watu wa Peponi, nao ni vijana na wazee, lakini kwa kutokana na kuwa Peponi hakuna wazee, hivyo basi Riwaya hii itakuwa na maana ya kwamba Wao (a.s) watakuwa ni mabwana wa watu wote wa Peponi, na hii ina maana ya kuwa Wao (a.s) watakuwa ni mabwana wa wale vijana wote, wawe wamekufa muhanga au wamekufa kwa ajali yao, na pia Wao (a.s) ni mabwana wa watu wa kawaida watakaokuwepo Peponi. Na hii kauli yenye kusema kuwa Wao (a.s) watakuwa ni pambo au ni mabwana wa wazee wa Peponi, inamaanisha wale waliokufa au kuuliwa muhanga kwa ajili ya Uislamu hali wakiwa katika umri mkubwa wa uzeeni, na hilo haliendi kinyume na ile kauli isemayo kuwa watu wa Peponi wote kwa ujumla waatakuwa katika umri wa ujana.
Swali jengine ambalo linaweza kuzaliwa ndani ya akili za baadhi ya watu, ni lile lisemalo kuwa: je Imamu Husein ana fadhila nyingi kuliko Mtume pamoja na Maimamu (a.s)? Jawabu ya swali hili inaweza kufahamika baada ya watu kufahamu kuwa: kila kitu kinapopewa sifa fulani, mara nyingi huwa haimaanishi kuwa sifa hiyo ni yenye kuhusiana na kitu hicho tu, na wakati mwingi hupatikana ufafanuzi wenye kuashiria jambo hilo ndani ya ile kauli yenye kukisifu kitu hicho, lakini baadhi ya wakati huwa hakupatikani ufafanuzi wowote ule wenye kuashiria jambo hilo ndani ya kauli yenye kukisifu kitu hicho, hii ni kwa kutokana na jambo hilo kuwa liko wazi mbele ya kila mwenye kufahamu na mwenye akili timamu.
Kwa hiyo natija makini inayoweza kufikiwa kupitia Riwaya hizi ni kwamba: Imamu Hasan na Husein (a.s) ni watukufu na ni mabwana wa wale watu wakawaida, na wala utukufu Wao (a.s) haukumzidi Mtume, Ali, Fatima na wengineo miongoni mwa Mitume na Maimamu (a.s).
Kwa ajili ya kuwafidisha zaidi wasomaji wa makala hii, mimi nimeamua kutoa nyongeza ya dalili kuhusiana na kipengele hichi cha mwisho, nayo kama ifuatavyo:
Mtu mmoja alikwenda kwa Imamu Sadiq (a.s) akamwambia: hivi Mtume wa Mola (s.a.w.w) kuhusiana na Abu-Dharri hakutoa bayana zilizosema kuwa yeye ndiye msema kweli zaidi?! Imamu Akamjibu ndio, yule mtu akasema: basi nafasi ya Mtume na Ali (a.s) imekwenda wapi katika kusema kweli?! Na nafasi ya Imamu Hasan na Imamu Husein (a.s) imekwenda wapi? (hivi Abu-Dharri ndiye msema kweli zaidi kuliko Wao (a.s))? Baada ya yule mtu kumaliza maneno yake, Imamu Sadiq (a.s) akamjibu kwa kusema: Sisi ni Ahulul-Bait hatuwezi kufananishwa na watu wengine wa kawaida, kwa hiyo Sisi tupo nje ya ulinganishaji wako huo.[3]
Inafahamika wazi kabisa katika Riwaya hii kuwa: Abu-Dharri amelinganishwa na watu wengine katika kusema kweli kwake, na wala ulinganishaji huo hauwezi kumuingiza Mtume na Maimamu (a.s) ndani yake, kwani ni jambo la wazi kuwa Mtume na Maimamu ni wenye kupambanuka na watu wengine kifadhila na kidaraja.
[1] Thawabul-aa’maal cha Sheikh Saduuq, uk/97, chapa ya Sharifur-Ridha, Qum Iran, mwaka 1364 Shamsia.
[2] Jarida la Sahifatur-Ridha (a.s), uk/30 la mwaka 1406 Hijiria.
[3] Maa’nil-akhbaar cha Sheikh Saduuq, juz/1, uk/179, chapa ya Jaamiatul-Mudarrisiin, Qum Iran, mwaka 1361 Shamsia.