advanced Search
KAGUA
9671
Tarehe ya kuingizwa: 2006/06/25
Summary Maswali
je kuna haja ya kumkhofu Mola au tunatakiwa kuwa na mapenzi Naye?
SWALI
je kuna haja ya kumkhofu Mola au tunatakiwa kuwa na mapenzi Naye?
MUKHTASARI WA JAWABU

Suala la mtu kuwa na khofu huku akiwa na matarajio ya kheri, na kwa upande wa pili akawa na mapenzi ya Mola wake, huwa si suala la kushangaza, kwa mambo hayo mawili hayapingani katika kuwepo kwake, kwani kuwepo kwa hali mbili kama hizo huwa ni jambo la kawaida ndani ya mambo mengi tunayokabiliana nayo maishani mwetu, na hata pale mmoja wetu anapoamua kukifuatilia kitu fulani, ndani ya ufuatiliaji wake huo huwa mnapatikana mapenzi au hamu ya kulifuatilia jambo hilo, na kama mtu atakosa kuwa na matarajio, hapo basi hatoweza yeye kukifuatilia hicho anachotaka kukifuatilia, na iwapo yeye hatokifuatilia, hapo basi hatoweza kulifikia lengo lake, na iwapo ataacha kuwa na khofu fulani juu ya kulifikia lengo lake, hapo basi hatokuwa na tahadhari, mtu asiyekuwa na tahadhari, wakati wowote ule anaweza kuharibikiwa njiani. Na hali kama hii inaonekana zaidi pale mtu anapokuwa anavitumia vifaa vya usafiri au nyenzo fulani zinzoambatana na masuala ya umeme na khadhalika. Na kila mmoja anapokuwa anavitumia vitu kama hivyo, huwa ana shauku kubwa ya kujifunza na kuelewa jinsi ya kuvitumia vitu kama hivyo, lakini iwapo mtu huyo ataacha kuwa na tahadhari, hapo basi anaweza akasababisha hasara kwa ajili ya nafsi yake pamoja na wengine. kinachotakiwa kueleweka basi ni kwamba: kwa upande mmoja mtu anatakiwa amuogope Mola wake, na kwa upande wapili anatakiwa kuwa na mapenzi kwa Mola wake. kwani  mambo mawili haya huwa ni yenye kumpa mtu msukumo wa kufanya jitihada zaidi za kutenda mema na kujisafisha, na hatimae kuweza kuzifikia fadhila za Mola wake Mtakatifu pamoja na kuzifikia neema za Mola wake, neema ambazo huwa ndio kiu ya kila mja duniani na Akhera. Na kwa upande mwengine, pale mtu anapomkhofu Mola wake, jambo hilo humpelekea yeye kumcha Mungu wake kwa umakini zaidi pamoja na kujiepusha na makatazo ya Mola wake, huku akijiepusha na yale yote yawezayo kumsababishia yeye kughadhibikiwa na Mola wake. Mtu kuwa na khofu kwa upande mmoja na akawa na matarajio kwa upande mwengine, huwa ndiyo msingi imara katika jamii ya watu wa kawaida, na hilo huwa linamsaidia yeye kuepukana na woga wa kukutana na Mola wake, pia huwa ni msingi wa kujisisikia yeye kuwa hana mzigo juu ya mgongo wake katika dunia hii pia kutarajia hesabu njema huko Akhera.

 

Dunia hii tuliomo ndani yake ni kama shamba ambalo tunatakiwa kulilima kwa ajili ya manufaa ya baadae, na kama inavyoeleweka kuwa kila shamba huwa linahitajia kushughulikiwa kisawa sawa ili mazao yake yaweze kuwa na manufaa zaidi, mazao ambayo huwa ndiyo rasilimali ya maisha ya baadae nayo ni maisha ya Akhera, na pale siku itakapowadia hapo basi hapatokuwa na haja tena ya kulilinda na kulihifadhi shamba hilo, kwani wakati wa kulima tayari umeshamalizika. Iwapo mtu atashikamana na khofu pamoja na woga tu hilo litamsababishia kunyongeka kwa roho yake pamoja na kuvunjika moyo, vile vile ashikamanaye na matarajio na matamanio ya huku akijidhatiti kuwa yeye atayafikia matarajio yake, huyo atakuwa anajidanganya na kuitamanisha nafsi yake bila ya msingi maalumu, jambo ambalo litaweza kusababishia yeye kutenda maasi kwa kutokana na matarajio pofu aliyonayo.

JAWABU KWA UFAFANUZI

Khofu na matarajio ni mambo yaliyomo moyoni yanayohisiwa na kila mmoja wetu, na mambo haya hayana haja ya kupewa ufafanuzi wa ziada kwa ni mambo yaliyo wazi kabisa katika ufahamikaji wake. Ni jambo lenye kuyumkinika kuwa mtu anapokabiliwa na jambo fulani, anaweza kupatwa na khofo au woga fulani. Kwa mfano iwapo mtu atakabiliwa na hatari ya kufilisika au kuuwawa, ni lazima mtu huyo aingiwe na khofu fulani, pia mtu anapokabiliwa na mtu fulani mwenye haiba au mwenye daraja ya juu, huwa ni mwenye kuingiwa na aina fulani ya khofu. Vile vile mtu anapoifikia natija ya tendo fulani alilolitenda pia huingiwa na khofu, khofu hiyo nayo huwa ni yenye kuongezeka kutoka hatua moja hadi nyengine, kwa jinsi ya ukubwa wa tendo hilo lilivyo. Fungamano la kimapenzi linalopatikana na kuhisiwa  ndani ya moyo wa mtu fulani, linaweza kupatikana kwa kutokana na sababu mbali mbali, na mingoni mwa sababu hizo ni kama ifuatavyo:

1- Kuvutiwa mtu na uzuri aliouhisi kuwepo ndani ya yule ampendaye, aina hii ya pendo huwa inasababishwa na ule uzuri aliouna na kuvutika nao, na inawezekana kwa mara moja au nyengine, likaonekana penzi hilo kupauka na kupoteza rangi yake ya mwanzo, lakini hali hiyo si yenye kuthibiti katika hali zote, bali inaweza kutokea iwapo uzuri huo utakuwa si uzuri wa kudumu bali ni uzuri wa mpito na wenye kufifia rangi yake, lakini ikiwa uzuri huo utakuwa ni uzuri wenye uhakika wa kudumu uliojengeka katika misingi ya kitabia iliyo thabiti, mapenzi yatakayoshikamana na uzuri wa aina hiyo hayatokuwa ni mapenzi ya mpito, bali kutapatikana fungamano litakalowafungamanisha baina ya mpenzi na mpendwa na kuwafanya kuwa ni kitu kimoja.

2- Na kwa mara nyengine mtu anaweze kufungamana na kitu fulani na kujenga upendo kwa kutokana na kukihitajia kitu hicho katika kuyafikia malengo yake, katika aina hii ya mapenzi, mpenzi mtu huwa anakipenda kitu fulani kwa ajili ya manufaa yake binafsi.

3- Pia mtu anaweza kukipenda kitu au mtu fulani kwa ajili ya manufaa na neema imfikiayo kutoka kwa mtu huyo, na mapenzi hayo huwa ni kwa ajili ya kuonesha shukurani zake kwa yule aliyemneemesha.

4- Mara nyengine mtu humpenda mtu fulani kwa ajili ya kujipendekeza, ili aweze kulichuma pendo la mtu huyo na kulilileta upande wake, kwa ajili ya kutafuta radhi pamoja na manufaa mbali mbali yatokayo kwa mtu huyo. Pia mtu anaweza kuwa na upendo na mtu fulani huku akiwa ana malengo tofauti katika upendo huo.

 

Iwapo tutafumbua macho kisawasawa, tutafahamu kuwa matendo yetu ya kila siku, huwa ni yenye kuchanganyika mno na hali mbali mbali za kimapenzi, matarajio pamoja na tamaa mbali mbali zinazotusukuma sisi katika kuyatenda matendo yetu ya kila siku. Ingawaje wakati mwengine upendo huwa uko mbele zaidi, na wakati mwengine tamaa ndiyo ikawa iko mbele, au pia khofu ndiyo ikawa imeshika hatamu katika utendaji wa jambo fulani, lakini bado mtu hatoweza kuepukana na moja kati ya mambo hayo. Lakini kwa kutokana sisi kuwa tunafanya kazi zetu bila kujiuliza kuwa ni kitu gani kinachotupa msukumo wa kufanya hivyo, mara nyingi basi sisi huwa hatukungundui siri za kiutendaji zinazotupa msukumo  katika utendaji wa matendo yetu.

Mapenzi na matarajio, huwa ndio msingi mkuu unaotupa nguvu za kiutendaji katika utendaji wa kazi zetu za kila siku, na khofu nayo huwa ndiyo jambo kuu linalotupa sisi msingi wa kuchukuwa tahadhari pale tunapofanya kitu fulani ambacho huwa kinatarajiwa kuleta madhara endapo tutaacha kuwa na tahadhari katika utendaji wa kitu hicho. Basi tungelikuwa sisi tunahitajia mapenzi na matarajio tu, huku khofu na tahadhari tukiziweka kando! hapo basi ingaliku ni rahisi sana sisi kuweza kutekete, na pia tungalikuwa sisi ni wenye kushikamana na khofu pamoja na thadhari! Basi tusingeweza kufanya chochote kile katika ulimwengu huu, na hata tungalikuwa tukiogopa kula na kunywa, kwa kukhofia kukwamwa na tonge au maji kupenya mapafuni mwetu, jambo ambalo huwa ni hatari kwa maisha ya mwanaadamu. Kwa hiyo sisi hatuoni kuwa kuna pingamizi yeyote ile iliopo baina ya mtu kumkhofu Mola wake huku akiwa na mapenzi na Mola huyo, lakini tatizo hasa tulilonalo sisi ni kule kuwa sisi hatujitambui vyema wala hatujamtambua Mola wetu ipaswavyo.

 

UFAFANUZI ZAIDI

Mapenzi, matarajio pamoja na khofu, huwa ni vyenye kutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwengine kwa jinsi ya watu hao wanavyotafautiana kielimu katika kumfahamu Mola wao, pia tofauti hizo hupatikana kwa kule kutofautiana kwao katika kuzifahamu sifa za Mola wao, kama vile sifa za uzuri na utukufu

(صفات جماليه و جلاليه) alizonazo Mola Mtakatifu. Elimu ya ufahamu wa dini kiujumla pamoja  na amali za watu pia huwa ni zenye kuchangia upatikanaji wa tofauti kutoka mtu mmoja hadi mwengine, tusisahau pia kuwa utulivu wa moyo katika kuwa na matumaini na maisha Akhera, huwa yana sehemu kubwa katika kuwatofautisha watu mbali mbali kiimani. Kwa hiyo kwa upande wa wale watu waliotenda maovu maishani mwao, khofu huwa ndiyo yenye kuchukua nafasi zaidi ndani ya nyoyo zao kuliko upendo, na kwa upande wa wale waliosafika tangu mwazo, upendo kwao ndio unaoshika hatamu ndani ya nyoyo zao. Na hata kama watu hawa watakuwa ni wenye kutenda baadhi ya makosa, lakini kwa kutokana na wao kuwa ni wema, basi huwa hawachelewi kurejea kwa Mola wao, hilo ni kwa kutokana na mapenzi yaliyojengeka baina yao na Mola wao. Kwa hiyo wale watu watendao maovu kisha wakatambua kuwa ni wenye kutenda maovu, iwapo watu hao watakuwa ni wenye kurudi kwa Mola wao, watu hao hawatoacha kuwa ndani ya mvutano ndani ya nafsi zao baina ya upendo na khofu kwa yale waliyoyatenda.

 

Mara nyingi utafiti umeonyesha kuwa muinuko wa kimapenzi pamoja na khofu zinazopatikana ndani ya nafsi za wanaadamu, chimbuko lake huwa ni kule mtu kuipenda nafsi yake na kuilinda kutokana na hatari zinazokadiriwa kutokea, pia suala hilo linasababishwa na kule mtu kujitakia manufaa ya nafsi yake, yaani wengi miongoni mwa wanaadamu humuabudu na kujenga mapenzi na Mola wa kwa kule kuwa na tamaa ya kupata fdhila za siku ya Kiama, au kutokana na khofu ya adhabu ambayo wanaikhofia kuwafika. Lakini kwa upande mwengine, kuna wale waja wanaomuabudu Mola wao kwa kutokana na kuzitambua vilivyo sifa za uzuri na utukufu alizonazo Mola wao, hao basi huwa ni wenye kumuabudu Mola Mtakatifu kwa kutokana na Yeye kuwa ni mwenye kustahiki kuabudiwa, nao ni wachache mno miongoni mwa waja wake, bali mara nyingi draja hiyo huwa inafikiwa na Mitume pamoja Mawalii wa Mola Mtakatifu.

 

Imam Ali (a.s) amewagawa wacha Mungu katika sehemu tatu kwa kusema: “Kuna kundi ambalo humuabudu Mola kwa tamaa ya kupata msamaha na tunuko mbali mbali, na hiyo ni ibada ya kibiashara, na kuna wengine wanaomuabudu Mola kwa kutokana na kumkhofu Mola wao, na hiyo ni ibada ya kitumwa au ya watumwa, na kuna kundi jengine la tatu linalomuabudu Mola wao kwa kuwa Yeye ni mwenye kustahiki kuabudiwa, na hiyo basi ndiyo ibada ya watu walio huru”[1]

 

Na usemi huo ndiyo uliyo wafanya baadhi ya wanazuoni kusema kuwa: “Moja kati ya misingi mikuu ya kimafunzo na kimalezi ndani ya Uislamu, ni kuleta upendo”. Qur-ani nayo ambayo ndiyo mwalimu wa na mfunzji mkuu wa masomo ya kitabia na kimaadili, imelitilia mkazo mno suala la upendo katika misingi ya kumjenga mtu kitabia na kimaadili. Imam Sadiq (a.s) naye anasema: “Mola Mtukufu alimlea na kumpa maadili Mjumbe wake (s.a.w.w) kwa kupitia njia ya upendo”[2].

 

Suala la kuwabashiria waja au kuwatahadharisha na adhabu pamoja na kuwatia shauku ya kutenda mema, zilikuwa ni kama nyenzo mbali mbali zilizotumika katika katika kuwaita watu katika njia iliyo sawa, ingawaje nyenzo hizo zilikuwa zikitumika kwa jinsi ya hali ya yule anayelinganiwa ilivyo.[3] Kwa hiyo yote mawili miongoni mwa khofu na upendo ni vyenye kuhitajika ndani ya jamii kwa jinsi hali za watu zilivyo, kwani mambo yote hayo mawili huwa ni nyenzo madhubuti zenye kumlea mwanaadamu na kumfikisha katika kilele cha darara za ubinaadamu, kwani mwanaadamu kwa kutokana na kuyaogopa yale yamkasirishayo Mola wake na kujiepusha nayo, huwa ni moja kati ya njia zimkaribishazo kwa Mola wake, na kwa upande wa pili upendo huwa unampelekea mja kutenda wajibu wake, pia kutenda yale yote anayodhania kuwa yanaweza kumpendekeza yeye mbele ya Mola wake. Na hayo ndiyo matakwa halisi Muumba wetu, kwani Yeye alimuumba mwanaadamu kwa matarajio ya mwanaadamu huyo kuwa karibu na Mola wake, ili aweze kusifika na sifa njema za Mola wake, jambo ambalo litamfanya yeye kuwa ni khalifa wa Mola ndani ya ardhi hii, na lengo la Mola ni kumuepusha mja wake na aina mbali mbali za khofu, kama lilivyosisitiwa jambo hilo katika Aya mbali mbali kuwa: “Mtu aliyemuamini Mola wake na kumuabudu kisha akafanya mema pamoja na kuiamini siku ya Kiama, huyo basi atapewa malipo makubwa mno mbele ya Mola wake, na walo mtu huyo hatofunikwa na khofu wa huzuni”.[4] Kwa kweli khofu si yenye natija isipokuwa ni yenye kuufisha moyo na kuutia huzuni pamoja nakuukatisha tamaa, jambo ambalo linaweza kumsababishia mtu kuacha kutubia mbele ya Mola wake, na hatimae kutumbukia ndini ya madhambi mbali mbali. Na uwande wa pili nao ndio hivyo hivyo, kwani iwapo mtu atakuwa na mapenzi uongo na kujidanganya kuwe yeye ni mpenzi wa Mola! Huyo naye hatoacha kuyapanda maovu na kuthubutu kutenda maasi kwa tamaa danganyifu aliyonayo, huku akijidanganya kuwa muda wa kutubia bado ungalipo kwa kujidai kua Mola ni mwenye upendo na huruma, Naye ni mtowaji wa taufiki kwa waja wake.

 

Imam Husein (a.s) amesema “Limepofuka jicho la yule adhaniaye kuwa Mola si mwenye kumuona, na hufilisika yule ambaye amekosa kupata upendo wako”

Basi ni biashara njema kwa wale waliopata upendo wa Mola wao ambao hawakuhadaika na dhana zao danganyifu za kusubiri mazao bila ya kulima, na khatari ilioje kwa wale waliodhania kuwa Mola ni mtoaji wa fadhila bila ya juhudi mtu mwenyewe, huku wakijidanganya kuwa bado wakati ungalipo, hao basi hawatoacha kulia na kuhuzunika baada ya kufahamu ukweli wa mambo yalivyo.

KWA AJILI YA KUTALII ZAIDI REJEA VITABU VIFUATAVYO:

1- Marahili akhlaq dar Qur-ani cha Ayatulla Jawadi Amuli/ uk: 279-340

2- Sherhe chehel hadithi cha imam Khomeini/ uk: 221-233, 481-484.

3- akhlaqi dar Qur-ani cha Taqiy Misbah Yazdi/ katika mlango wa khofu na matarajio (بحث خوف و رجاء)

 

 


[1] Tarjuma ya Nahjul-Balagha ya Muhammad dashti/ hekima ya 237/ uk: 678.

[2] Biharul-Anwar/juz: 17/ uk: 3.

[3]Kitabu Marahilul-Akhlaaq dar Qur-ani  Abdul-lahi Jawadi amuli/ uk: 330-332.

[4] Suratul-Baqara Aya ya 62/ na suratul-Maaida Aya ya 65.

 

TARJAMA YA JAWABU KATIKA LUGHA NYENGINE
MAONI
Idadi ya maoni 0
Tafadhali ingiza thamani
mfano : Yourname@YourDomane.ext
Tafadhali ingiza thamani
<< Niburute.
Tafadhali ingiza kiasi sahihi ya usalama Kanuni

MPANGILIO WA KIMAUDHUI

MASWALI KIHOLELA

YALIYOSOMWA ZAIDI